Viongozi wa Ulaya kuendelea kuiunga mkono Ukraine
3 Machi 2025Mkutano huo uliofanyika siku ya Jumapili mjini London na kuwaleta pamoja viongozi wa mataifa 18 ya Ulaya, ulifanyika siku mbili tu baada ya majibizano makali kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliyekuwa ziarani mjini Washington.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya watashirikiana na Ukraine kuhusu mpango wa kusitisha mapigano, ambao baadaye utawasilisha kwa Marekani, ambaye ni mshirika wao mkuu licha ya kuwa misimamo yake kwa sasa imekuwa ya kutiliwa mashaka kama alivyosisitiza Starmer kwamba kwa sasa Ulaya ipo njia panda.
Waziri mkuu huyo wa Uingereza alisisitiza kuwa huu si wakati wa mazungumzo zaidi bali ni wakati wa kuchukua hatua za kuunga mkono mpango mpya wa amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine lakini akasisitiza kuwa bila dhamana ya usalama ya Marekani, Ulaya italakazimika kufanya kazi kubwa.
Soma pia: Viongozi wa Ulaya wanakutana London kujadili migogoro
Zelensky amesema hii leo kuwa yuko tayari kushirikiana na mataifa ya Ulaya ili kuandaa mpango huo wa amani na kuuwasilisha kwa Washington.Aidha, Zelensky ameishukuru Marekani kwa msaada wake, baada ya kushambuliwa Ijumaa na Makamu wa rais JD Vance kuwa mwizi wa fadhila.
" Diplomasia itazingatiwa kwa ajili ya amani na kwa ajili ya umoja wetu: Ukraine, Ulaya, na bila shaka tutaijumuisha Marekani. Tunaufahamu umuhimu wa Marekani, na tunashukuru kwa msaada wote tuliopokea kutoka Marekani."
Mataifa ya Ulaya yadhihirisha mshikamano
Malumbano kati ya Trump na Zelensky yalizusha pia maswali mapya kuhusu dhamira ya Marekani kwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, lakini Katibu Mkuu wa muungano huo wa kijeshi Mark Rutte amesema anaamini kuwa Marekani itaendelea kuwa mshirika wa kuaminika akisema mataifa yote yanatakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa amani nchini Ukraine.
Mazungumzo ya Jumapili mjini London ambayo yameonekana kama ya kumfariji Zelensky baada ya kushambuliwa na Trump, yamefanyika katika wakati ambapo Ukraine ikiendelea kukabiliana na mashambulizi makali ya Urusi huku uungwaji mkono wa Marekani ukiwa mashakani. Wachambuzi wanasema yote haya, yamepelekea mataifa ya Ulaya kuungana na kudhihirisha mshikamano zaidi.
(Vyanzo: AP, AFP, Reuters, DPA)