Viongozi wa Thailand na Cambodia kufanya mazungumzo ya amani
27 Julai 2025Hayo ni baada ya nchi hizo jirani kuendelea kushambuliana katika mzozo uliosababisha vifo vya watu 34 na wengine zaidi ya 200,000 wakiyahama makazi yao.
Kaimu Waziri Mkuu wa Thailand Phumtham Wechayachai na Waziri Mkuu wa Cambodia Hun Manet watakutana mjini Kuala Lumpur kwa mazungumzo chini ya upatanishi wa kiongozi wa Malaysia Anwar Ibrahim, ambaye ndie mwenyekiti wa sasa wa jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi na kiusalama ya nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN ambayo Thailand na Cambodia ni wanachama.
Mazungumzo hayo yameshinikizwa pia na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye Jumamosi usiku alizungumza na viongozi wote wawili na kusema wamekubali "kutatua haraka tofauti zao" na kufikia mpango wa usitishaji mapigano. Cambodia na Thailand zinazozania eneo la mpakani linalopatikana kaskazini mashariki mwa mataifa hayo.