Viongozi wa NATO na Ulaya wataka ushirikiano zaidi
24 Juni 2025Viongozi hao aidha wameonyesha dhamira ya kujiimarisha kijeshi kukabiliana na hujuma zozote kutoka kwa Urusi kwa kuongeza bajeti yake ya ulinzi.
Akizungumza katika Kongamano la Sekta ya Ulinzi ya NATO linalofanyika kabla ya mkutano wa kilele wa siku mbili wa NATO mjini The Hague Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte amesisitiza umuhimu wa uhusiano thabiti kati ya NATO na Marekani na sekta ya ulinzi imara ili kudumisha amani.
Amesema NATO inapaswa kuchukua hatua zaidi kuimarisha bajeti yake ya ulinzi na haipaswi kukubali kushindwa na Urusi.
''Hivyo tunahitaji kuondoa vizuizi na kuhimiza ushirikiano wa kweli wa kiulinzi kati ya Marekani na Ulaya. Ni Ulaya na Amerika Kaskazini pekee ndizo zinaweza kuinuka na kukabiliana na changamoto hiyo. Kuna msemo wa Kirumi unasema, kama unataka amani, jiandae kwa vita. Ni jambo rahisi. Imarisha ulinzi wako hadi asiwepo mtu anayeweza kuthubutu kukushambulia.''
NATO yasisitiza kuendelea kuisadia Ukraine
Katibu huyo Mkuu wa muungano huo wa kijeshi, amebainisha kuwa viongozi wa NATO wanakaribia kuchukua hatua ya kihistoria kutoa rasilimali zinazohitajika kwa ulinzi imara. Amemuhakikishia Rais Zelensky kuwa anaweza kutegemea kuendelea kuungwa mkono na washirika kwa ajili ya ulinzi wake dhidi ya Urusi.
Kwa upande wake Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amepongeza kile alichokiita ahadi ya kihistoria ya matumizi ya NATO, akisema sekta ya ulinzi ya Ulaya ''hatimaye imeamka''.
''Kesho mkutano wa kilele utaweka malengo mapya ya kihistoria ya matumizi kwa washirika wa NATO. Lakini jinsi tunavyowekeza ni muhimu sawa na kiasi tunachowekeza.''
Von der Leyen amesema katika miezi ya hivi karibuni Ulaya imechukua hatua ambayo ilionekana kutofikirika mwaka mmoja uliopita.
Rais Zelensky kukutana tena na Trump
Katika hatua nyingine Rais Zelensky amewatolea wito washirika wake wa NATO kuongeza uwekezaji katika uzalishaji wa silaha kwa Ukraine na kudhibiti vifaa kutoka nje vinavyotumiwa na Urusi katika kutengeneza silaha zake. Zelensky amesema wanapaswa kuhakikisha kwamba uwezo wao wa ulinzi na uwezo wa washirika wake unafanya kazi kwa ajili ya amani yao, na sio kwa ajili ya wazimu wa Urusi.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump, amesema huenda atakutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pembezoni mwa mkutano wa kilele wa NATO. Akizungumza kwenye ndege yake Air Force One, Trump amesema Zelensky yuko katika wakati mgumu ambao hakupaswa kuupitia.