Viongozi wa kanisa Kongo wakutana na waasi wa M23
13 Februari 2025Ujumbe huo wa pamoja kutoka Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kongo na ule wa Kanisa la Kristo la Kongo uliwasili Goma siku ya Jumatano na kukutana na kiongozi wa kisiasa wa kundi la M23, Corneille Nangaa.
Nangaa amekuwa alama ya uongozi wa kundi hilo tangu lilipoukamata mji muhimu mashariki mwa Kongo wa Goma mwishoni mwa mwezi Januari.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu la Kongo, Askofu Donatien Nshole, amesema mkutano na M23 ulikuwa nafasi ya kutafuta njia za kumaliza vita haraka iwezekanavyo. Amesema taasisi hizo mbili kubwa za kidini zinaamini mzozo unaoendelea nchini humo hautamalizwa kwa njia za kijeshi.
Mkutano huo umefanyika wakati inaarifiwa waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda wanaendelea na mapigano wakisonga mbele kuelekea mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini wa Bukavu.