Viongozi wa Afrika Mashariki kuijadili hali Congo
8 Februari 2025Viongozi wa nchi wa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakutana jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kuujadili mgogoro wa Congo. Rais wa Rwanda Paul Kagame anatarajiwa kukutana na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi katika mkutano huo utakaowaleta pamoja pia viongozi wa mataifa wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya kusini mwa Afrika, SADC.
Mkutano wa Dar es Salaamu unafanika siku moja tu baada ya jeshi la Congo kukanusha madai ya Rwanda kuikalia sehemu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, huku machafuko yakiendelea kupamba moto mashariki mwa Congo. Luteni Jenerali Masunzu Pacifique, kamanda wa kikosi cha eneo la tatu la ulinzi amesema katika taarifa iliyosomwa na msemaji wake Meja Nestor Mavudisa Kamba Mayoyo kwamba jeshi limejiandaa kuhakikisha usalama wa raia na kuilinda mipaka ya nchi.
"Ziara hii katika eneo zima la mapambano inalenga kufikisha mwisho tetesi zinazoenezwa na adui, kutumia uongo kudai kwamba jeshi la Rwanda na washirika wake waasi wa M23 wamelidhibiti eneo hili la kiutawala. Jeshi la Congo FARDC liko tayari kikamilifu na linaendelea kuhakikisha usalama wa raia wote bila ubaguzi, pamoja na ulinzi wa mipaka ya nchi."
"Hakuna hata sentimita moja ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itakayokabidhiwa kwa jeshi la Rwanda na washirika wake kutoka muungano wa AFC na M23," aliongeza kusema Mayoyo.
Mayoyo amewatolea wito wakaazi wa jimbo la Kivu Kusini, hususan wa mji wa Bukavu, waendelee kuwa watulivu na wawe na imani na jeshi lao halali la FARDC. Amemhimiza kila raia apuuze taarifa za uongo zinazoenezwa na adui wa jamhuri katika mitandao ya kijamii na wasizisambaze katika mfumo wowoe ule.
Mayoyo amewashukuru raia wa Congo wa kila tabaka la maisha, ambao wamejitolea kwa dhati kwa ajili ya amani na wanaoliunga mkono jeshi lao kwa njia mbalimbali.
Soma pia:Congo yataka ukiukwaji wa haki uchunguzwe Goma
Katika mkutano wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa uliofanyika mjini Geneva hapo jana, kamishna mkuu anayeshughulikia masuala ya haki za binadamu Volker Turk alitahadharisha kuhusu unyanyasaji wa ngono kuendelea kuwa mbaya mashariki mwa Congo. Alihimiza hatua za haraka zichukuliwe kuepusha mgogoro kuendelea kuwa mbaya zaidi.
Congo imeidhinisha tume maalumu ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki, huku ripoti ikitarajiwa kukamilika Septemba 2025. Rwanda imekanusha kuwa na dhamana katika mkutano huo, ikidai ushahidi wa shambulizi kubwa lililopangwa na Congo.
Nchi za katikati mwa Afrika zataka machafuko yakome Congo
Wakati hayo yakiarifiwa, mataifa ya katikati mwa Afrika yametoa wito makubaliano ya kusitisha mapigano yafikiwe kati ya Congo na Rwanda. Viongozi wa mataifa hayo wamelilaani kwa nguvu kundi la M23 na kuwataka wasitishe vita mara moja.
Akizungumza baada ya mkutano wa dharura wa baraza la amani na usalama la Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika ya Kati ECCAS yenye nchi 11 wanachama, mjini Malabo, Rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang amesema jumuiya hiyo imetaka mapigano yakome mara moja kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Obiang amesema kwa sasa jumuiya yao inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa usalama unaoziathiri nchi mbili wanachama, Congo na Rwanda, ambazo zinakabiliwa na vita vilivyosababisha mgogoro wa kutisha wa kibinadamu katika eneo lao.
"Kama mwenyekiti wa muda wa Jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika ya Kati, ninatoa wito wa mdahalo wenye tija, kuheshimiwa kwa uhuru na mipaka ya mataifa na nazitaka pande husika katika mgogogoro huu zionyeshe mazingira mazuri ya ushirikiano kuwezesha njia za amani zilizopendekezwa katika mchakato wa Luanda."
Obiang ameongeza kusema, ili kuhakikisha mgogoro huu hauenei katika maeneo mengine, wanatoa wito mapigano yasitishwe mara moja ili kushughulikia vyanzo msingi vinavyozuia maelewano mema kati ya nchi hizi mbili. Rais huyo wa Guinea ya Ikweta aidha alisema mgogoro wa Congo unawalazimu kuchukua hatua za haraka ili kuzuia athari za mzozo huu wa kivita, ili kuuzuia kuwa mbaya zaidi kutokana na makabiliano ambayo yanazidisha hali ya kibinadamu kuwa mbaya, inayozidi kuwa vigumu kushughulikiwa.
Wakuu wa nchi za ECCAS wametaka vikosi vya Rwanda viondoke mara kutoka kwa ardhi ya Congo na eneo maalumu litengengwe kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kibinadamuili kuwezesha misaada kupelekwa katika eneo la vita mashariki mwa Congo.