Viongozi wa G7 wakutana Canada
16 Juni 2025Viongozi wa nchi tajiri kiviwanda duniani za kundi la G7 wanakutana nchini Canada kwenye mkutano wa kilele katikati ya kiwingu cha vita kati ya Iran na Israel na Urusi na Ukraine.
Rais wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa viongozi ambao wamewasili kushiriki mkutano huo katika nchi ambayo alitishia kuinyakuwa kwa nguvu.
Kansela wa Ujerumani, Freidrich Merz, kabla ya kuelekea Canada jana Jumapili, aliwaambia waandishi wa habari kwamba mgogoro wa Israel na Iran unatarajiwa kugubika mkutano huo wa kilele.
''Hatua iliyopiga Iran kuelekea kujipatia silaha za nyuklia ndiyo iliyoifanya Israel kuyalenga maeneo ya Iran katika mashambulizi yake ya kijeshi siku ya Ijumaa. Suala hili litagubika ajenda za mkutano wa kilele wa G7. Lengo langu litakuwa ni kuhakikisha yanafikiwa makubaliano juu ya vipengele vinne. Kwanza na kipengele muhimu ni Iran lazima izuiwe kutengeneza au kumiliki silaha za nyuklia.''
Umoja wa Ulaya na washirika wengine ambao sio wanachama wa G7 pia wanashiriki mkutano huo wa kilele akiwemo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ambaye amesema anapanga kujadiliana na Rais Donald Trump, juu ya mpango mpya wa kununua silaha pembezoni mwa mkutano huo.