Viongozi wa EU walaani mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine
7 Septemba 2025Rais wa Halmashauri ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Kremlin "inadhihaki diplomasia, inakanyaga sheria za kimataifa na inaua kiholela,” huku Rais wa Baraza la Ulaya António Costa akiongeza kuwa kuzungumzia amani wakati mashambulizi yakiendelea ndiyo tafsiri ya Putin ya amani.
Maafisa wa Umoja huo wamesema maandalizi ya awamu ya 19 ya vikwazo vipya dhidi ya Moscow yanaendelea na yanatarajiwa kuhitimishwa katika siku chache zijazo kabla ya kuidhinishwa na nchi 27 wanachama.
Hatua zinazozingatiwa ni pamoja na nyongeza za ushuru na marufuku ya bidhaa zaidi kutoka Urusi, pamoja na vikwazo kwa wahusika wa nchi nyingine wanaonufaika na vita vya Kremlin.
Aidha, Brussels inapanga kuchukua mkakati mkali zaidi dhidi ya kile kinachoitwa meli za kivuli za Urusi zinazokwepa vikwazo vya nishati, sambamba na hatua mpya kwa sekta ya fedha na udhibiti wa miamala kupitia sarafu za kidijitali.