Viongozi wa EU waafikiana kuongeza matumizi ya ulinzi
7 Machi 2025Hayo yametangazwa jana wakati wa mkutano wao wa kilele uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini Brussels-Ubelgiji, hatua iliyochukuliwa baada ya miongo kadhaa ya kusuasua.
Aidha, nchi 26 za Umoja wa Ulaya zilitoa tamko la pamoja la mshikamano na Ukraine lakini Hungary ilikataa kutia saini nyaraka hiyo.
Soma pia: Waziri Mkuu wa Ureno kujiuzulu kufuatia kashfa ya ufisadi?
Rais wa Baraza Kuu la Umoja huo, Antonio Costa, amesema Ulaya kwa sasa imedhamiria kusonga mbele pamoja kwa ajili ya ulinzi wake na itaendelea kushikamana na Ukraine.
"Sote tunataka amani. Tofauti ni kwamba nchi 26 zinaamini kuwa njia ya amani ni kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa Ukraine. Hungary imejitenga na makubaliano haya na inasimama peke yake. Nchi moja pekee haileti mgawanyiko. Nchi zingine 26 zinabaki na msimamo mmoja na zitaendelea kuiunga mkono Ukraine, kama tulivyofanya tangu siku ya kwanza ya uvamizi mnamo Februari 24, 2022. Tutaendelea hivo."
Hatua hii kwa sehemu kubwa imechangiwa na mashaka yanayoongezeka kwamba Marekani iliyo mshirika wa siku nyingi wa nchi za Ulaya inabadili mwelekeo wake tangu kurejea madarakani kwa rais Donald Trump, ambaye amerejea kusema hapo jana kuwa nchi zisizotoa mchango wa kutosha kwenye Jumuiya ya Kujihami ya NATO hazistahili kupewa ulinzi.