Viongozi wa dunia walaani shambulio la Urusi Ukraine
14 Aprili 2025Viongozi wa dunia wamelaani vikali Urusi kwa shambulizi la makombora dhidi yamji wa Sumy, kaskazini mashariki mwa Ukraine, lililotokea Jumapili asubuhi na kuwaua watu wasiopungua 34 huku wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa. Hili ni mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi tangu kuanza kwa vita. Rais wa Marekani Donald Trump alilitaja tukio hilo kuwa ni "jambo la kutisha" na "kosa."
Kwa mujibu wa mamlaka za Ukraine, makombora mawili ya masafa marefu yalilenga katikati mwa jiji hilo lililo karibu na mpaka wa Urusi. Shambulizi hilo lilijiri siku mbili tu baada ya mjumbe maalum wa rais wa Marekani, Steve Witkoff, kusafiri kwenda Urusi kukutana na Rais Vladimir Putin kwa lengo la kuendeleza juhudi za Trump kusitisha vita hivyo vya zaidi ya miaka mitatu.
"Nadhani lilikuwa tukio baya sana. Niliambiwa walifanya kosa. Lakini ni jambo la kutisha. Vita vyenyewe ni jambo la kutisha,” alisema Trump akiwa njiani kurejea Washington ndani ya ndege ya Air Force One.
Alipoulizwa afafanue alichomaanisha kwa kusema "kosa", Trump alijibu: "Walifanya kosa… utakwenda kuwauliza wao," bila kufafanua alikuwa anamaanisha nani hasa.
Wito wa Zelensky kwa Trump na majibu ya kimataifa
Wakati huo huo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alimtaka Trump kufika Ukraine ili ajionee mwenyewe uharibifu unaosababishwa na uvamizi wa Urusi.
"Tafadhali, kabla ya kufanya maamuzi yoyote au kuanza mazungumzo ya aina yoyote, njoo uone watu, raia, wapiganaji, hospitali, makanisa, watoto waliouawa au kuharibiwa,” alisema katika mahojiano yaliyotangazwa na kituo cha CBS.
Soma pia: Watu zaidi ya 30 wauawa na wengine 80 wajeruhiwa kwenye shambulio la Urusi
Zelensky alisisitiza kuwa shambulizi hilo lilitokea katika Jumapili ya Matawi (Palm Sunday), siku muhimu kwa Wakristo. "Ni watu waliopoteza akili kabisa wanaoweza kufanya jambo kama hili,” aliongeza katika hotuba yake ya jioni.
Idara za huduma za dharura zilisema kuwa miongoni mwa waliouawa ni watoto wawili, na waliojeruhiwa walifikia 117 wakiwemo watoto 15. Watu walikimbia kujificha huku magari yakiteketea kwa moto na miili ikiwa imetalazwa chini kwa karatasi za rangi ya fedha. Zelensky alisema watu wanane waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.
Majengo 20 yakiwemo chuo kikuu, majengo matano ya makazi, mikahawa, maduka na mahakama ya wilaya yaliharibiwa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kushtushwa na tukio hilo akisema ni muendelezo wa mashambulizi yenye uharibifu mkubwa dhidi ya miji ya Ukraine katika wiki za hivi karibuni.
Makombora ya kisasa, mashahidi na siasa za vita
Mkuu wa ujasusi wa kijeshi wa Ukraine (GUR), Kyrylo Budanov, alisema kupitia Telegram kuwa Urusi ilitumia makombora ya kisasa aina ya Iskander-M/KN-23. Mmoja wa mashahidi aliyezungumza na shirika la habari la AFP alisema alisikia milipuko miwili: "Watu wengi walijeruhiwa vibaya sana. Kulikuwa na miili mingi.”
Hili ni shambulizi la pili mwezi huu lililosababisha vifo vya raia wengi. Awali, mashambulizi kwenye mji wa Kryvi Rig – nyumbani kwa Zelensky – yaliwaua watu wasiopungua 18, wakiwemo watoto tisa.
Trump anaendelea kushinikiza kumalizika kwa vita hivi kwa haraka, huku Marekani ikiendesha mazungumzo ya moja kwa moja na Urusi licha ya mashambulizi haya kuendelea.
Soma pia: Urusi na Uturuki zaijadili mizozo ya Ukraine, Mashariki ya Kati
Washington pia imefanya mazungumzo na maafisa wa Ukraine kuhusu uwezekano wa kusitisha mapigano, wakati nchi za Ulaya zikijadili uwezekano wa kupeleka vikosi vya kijeshi kusaidia usitishaji wa mapigano.
Hapo awali, Kyiv ilikubali pendekezo la Marekani la usitishaji mapigano usio na masharti, lakini Urusi ililikataa. Zelensky ameitaka Marekani na Ulaya kutoa "majibu makali” kwa Urusi, akiongeza kuwa: "Mazungumzo hayawezi kuzuia makombora na mabomu.”
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema shambulizi la Sumy linaonesha dharau kubwa ya Urusi kwa maisha ya watu, sheria za kimataifa na juhudi za kidiplomasia za Rais Trump.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema ameshtushwa na shambulizi hilo, huku mwenzake wa Italia, Giorgia Meloni, akilitaja kama "kitendo cha woga.”
Kansela mtarajiwa wa Ujerumani, Friedrich Merz, ameliita shambulizi hilo kuwa "uhalifu mkubwa wa kivita, wa makusudi na wa kudhamiria.”
Urusi imeendelea na mashambulizi dhidi ya Ukraine katika wiki za hivi karibuni, huku mji wa Sumy ukiwa chini ya shinikizo zaidi tangu Urusi kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Ukraine kutoka mkoa wa Kursk, upande wa Urusi.
Kyiv imekuwa ikionya kwa wiki kadhaa kuwa huenda Urusi ikaanzisha mashambulizi mapya dhidi ya jiji hilo. Jumapili, Urusi ilitangaza kuwa imeteka kijiji kingine mashariki mwa Ukraine katika eneo la Donetsk.
Chanzo: Mashirika