Majibizano kati ya Trump na Zelensky yaendelea kuwa gumzo
1 Machi 2025Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Canada, Uingereza wamesema wataendelea kusimama na Ukraine. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameikosoa kauli ya Trump kwa Zelensky kuwa anacheza na uwezekano wa kutokea Vita vya Tatu vya Dunia.
" Iwapo kuna mtu yeyote anayetishia Vita vya vya Tatu vya Dunia, jina lake ni Vladimir Putin. Yeye ndiye aliyeanzisha vita vya uchokozi miaka mitatu iliyopita na ndiye aliyeleta wanajeshi 10,000 wa Korea Kaskazini kwenye ardhi ya Ulaya. Ndiye aliyeleta droni kutoka Iran ili kuwasaidia katika mpango wao wa nyuklia, na kuzihusisha kwenye mapigano katika ardhi ya Ulaya. Huyu ndiye mtu ambaye ameendeleza uchochezi na kuihusisha China. Yaani kama kuna mtu ambaye sote tumesikia akitutishia kwa silaha za nyuklia na kucheza na uwezekano wa kutokea vita vya tatu vya dunia, mtu huyo usimtafute Kiev, mtafute huko Moscow."
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema Ukraine inaweza kuitegemea Ulaya. Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ambaye kesho ameandaa mkutano wa kilele wa mataifa ya Ulaya mjini London amesema wataendelea kuiunga mkono Ukraine na kufanya kila liwezekanalo ili kuelekea kwenye amani ya kudumu.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni ametahadharisha kuwa mgawanyiko wa mataifa ya Magharibi haumfaidishi yeyote bali huwafanya kuwa dhaifu. Urusi kwa upande wake imesema ziara ya Zelensky huko Marekani imeonyesha "kushindwa" kwa diplomasia ya Kiev.