Mwili wa Rais wa zamani wa Ujerumani Köhler kuagwa leo
18 Februari 2025Viongozi wakuu wa kisiasa nchini Ujerumani wanatarajiwa kukusanyika leo kwa ibada ya kumuaga rais wa zamani Horst Köhler mjini Berlin. Köhler alifariki dunia mapema mwezi huu akiwa na umri wa miaka 81. Alichaguliwa mwaka wa 2004 kuwa rais wa tisa wa Ujerumani, akimrithi Johannes Rau.
Soma: Rais wa zamani wa Ujerumani Horst Köhler amefariki dunia
Köhler alichaguliwa tena kwa muhula wa pili mwaka wa 2009. Kujiuzulu kwake mara moja mwaka mmoja baadaye ni hatua ambayo haikuwahi kushuhudiwa katika historia ya jamhuri hiyo ya shirikisho. Alikuwa rais wa kwanza ambaye hakuwa mwanasiasa wa vyama bali alitokea kwenye sekta ya kibiashara. Katika ibada ya kumuaga itakayofanyika kwenye Kanisa Kuu la Kiinjili la Berlin, Rais aliyeko madarakani Frank-Walter Steinmeier, rais wa zamani wa Austria Heinz Fischer na waziri wa zamani wa fedha wa Ujerumani Theo Waigel watahutubia.