Viongozi EU wakutana kuijadili Ukraine na usalama wa Ulaya
6 Machi 2025Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanashiriki katika mkutano wa dharura mjini Brussels, kwa lengo la kuimarisha usalama wa umoja huo pamoja na taifa la Ukraine. Mkutano wa Brussels unazikutanisha nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alipokutana na Rais wa Marekani Donald Trump katika mkutano ulioparaganyika bila muafaka.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaohudhuria mkutano huo mjini Brussels nchini Ubelgiji wamesema wataendelea kusimama na Ukraine na kuongeza matumizi katika ulinzi kutokana na mambo kubadilika baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kubadilisha sera za Marekani mara tu alipoingia madarakani.
Soma zaidi:Viongozi wa Ulaya kuendelea kuiunga mkono Ukraine
Rais wa Halmashauri Kuu ya umoja huo Ursula von der Leyen amesema Ulaya inakabiliwa na kitisho cha wazi hivi sasa na kwamba Ulaya inapaswa kuwa na uwezo wa kujilinda yenyewe. Von der Leyen ameshaandaa mpango wa euro bilioni 800 wa kuijenga kijeshi Ulaya unaoyataka mataifa kuongeza zaidi matumizi ya ulinzi. Mpango huo unatarajiwa kuidhinishwa katika mkutano huo.
Viongozi wanaoshiriki kwenye majadiliano hayo wanatazamiwa pia kuanza kutoa hakikisho la usalama kwa ajili ya makubaliano ya amani ya Ukraine ikiwemo uwezekano wa kupelekwa kwa wanajeshi wa Ulaya suala ambalo baadhi ya nchi zinalikubali.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliyewasili mjini Brussels kushiriki kwenye mkutano huo amewashukuru viongozi wa Umoja wa Ulaya kwa kuonesha mshikamano na nchi yake.
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, amesisitiza umuhimu wa Ulaya kuiunga mkono Ukraine kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO ili kujihakikishia ulinzi.
Wazo la Macron la kutumia silaha la nyuklia za Ufaransa laibua hisia tofauti
Hata hivyo, scholz ameonesha wasiwasi juu ya kauli ya Jumatano iliyotolewa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyependekeza wazo la kutumia silaha za nyuklia za Ufaransa ili kuzilinda nchi nyingine za Ulaya dhidi ya vitisho vya Urusi.
Licha ya wasiwasi wa Scholz tamko hilo limeungwa mkono na Poland na mataifa ya eneo la Baltiki wakati Urusi ikitaja suala hilo kuwa ni uchockozi uliopindukia.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, amesisitiza wito kwa Ulaya kujilinda dhidi ya Urusi akisema hilo linapaswa kuwa moja ya vipaumbele vya umoja huo kwa kuratibu uwezo wa mataifa kujenga jeshi moja lililoratibiwa vyema.
Poland, nchi mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO ambayo ni jirani na mshirika muhimu wa Ukraine inapakana pia na Urusi na Belarus yenye ushirika wa karibu na Moscow.
Naye Waziri Mkuu wa Hungary Victor Orban, anayeshiriki pia katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya amesema licha ya kutofautiana na viongozi wenzake wa Ulaya mara kwa mara, Ulaya inapaswa kuimarisha uwezo wake wa ulinzi.