Viongozi duniani wampongeza Merz kwa ushindi
24 Februari 2025Rais wa Marekani, Donald Trump ni mmoja wa viongozi waliompongeza Merz, licha ya kiongozi huyo wa CDU/CSU kujitenga na Marekani. Katika hotuba yake jana usiku kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth, Rais Trump alimpongeza Merz na wale wote waliouchagua muungano huo wa kihafidhina.
Trump alisema kama vile Marekani, watu wa Ujerumani walichoshwa na ajenda ya kutokuwa na mtazamo wa kawaida, hasa kuhusu nishati na uhamiaji.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameandika katika mtandao wa kijamii wa X, kwamba nchi yake inatazamia kuendelea na kazi yao ya pamoja na Ujerumani kuyalinda maisha ya watu, kuleta amani ya kweli Ukraine na kuliimarisha bara la Ulaya. Merz ameweka bayana kuwa kipaumbele chake ni kuileta Ulaya pamoja,
Soma: Uchaguzi wa Ujerumani: Matokeo yaawali yaonyesha CDU/CSU waongoza
Aidha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Mark Rutte pia amempongeza Merz kupitia mtandao wa kijamii wa X, kwa ushindi alioupata na amesema anatazamia kufanya kazi na kansela huyo ajaye katika wakati huu muhimu kwa usalama wao pamoja.
Kwa upande wake, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, nchi jirani na mshirika muhimu wa Ujerumani, amempigia simu Merz na kumpongeza. Macron amesema wamedhamiria zaidi kuliko awali kufanya mambo makubwa kwa pamoja kwa ajili ya Ufaransa na Ujerumani, na kufanya kazi kuelekea kuwa na Ulaya yenye nguvu na uhuru.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu naye amempongeza Merz kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, akisema anatazamia kufanya kazi kwa karibu na serikali ijayo ili kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer pia ametuma salama za pongezi kwa Merz na muungano wa CDU/CSU, akisema anatazamia kufanya kazi na serikali mpya kuimarisha uhusiano imara wa nchi hizo mbili, ambao tayari uko, pamoja na kuimarisha usalama wao wa pamoja na kuzikuza Uingereza na Ujerumani.
Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez pia hakubaki nyuma kumpongeza Merz kwa ushindi alioupata. Sanchez amesema Ulaya yenye nguvu inahitaji kufanya kazi kwa kushirikiana pamoja ili kukabiliana na changamoto zinazofanana.
Naye kiongozi wa Chama cha Kihafidhina cha Watu cha Austria, Christian Stocker amempongeza Merz kwa ushindi alioupata. Stocker amesema kama ilivyo kwa Austria, Ujerumani inakabiliwa na changamoto nyingi, na kwa wakati kama huu, hatua madhubuti na kuimarisha eneo la kibiashara inabidi kuwa ajenda ya sasa.
Mfumo wa uchaguzi wa Ujerumani: Uchaguzi wa Bundestag: Ujerumani imepiga vipi kura?
Viongozi wengine waliompongeza Merz ni pamoja na Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Czech, Petr Fiala.
Wakati huo huo, Makamu Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Salvini amesema mabadiliko yameshinda pia Ujerumani. Salvini amempongeza kiongozi mwenza wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD, Alice Weidel, baada ya chama chake kujiimarisha zaidi na kushika nafasi ya pili kutokana na kuongeza maradufu kura zake. Salvini amemtaka Weidel kuzuia uhamiaji haramu, kuweka kipaumbele katika amani na ajira.