Vikwazo vya Trump dhidi ya Karim Khan vyakwamisha kazi ICC
15 Mei 2025Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imekumbwa na hali tete baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuiwekea vikwazo, hali ambayo imeathiri utendaji wake kwa kiwango kikubwa. Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Karim Khan, amepoteza matumizi ya barua pepe na akaunti zake za benki zimefungwa.
Wafanyakazi wa Marekani ndani ya mahakama hiyo wameonywa kuwa wakirejea nchini kwao, wanaweza kukamatwa. Baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yamesitisha ushirikiano na mahakama hiyo, huku viongozi wake hata wakikwepa kujibu barua pepe kutoka ICC.
Kwa mujibu wa mahojiano na maafisa wa sasa na waliowahi kufanya kazi ICC, pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu, vikwazo hivyo vimezuia juhudi za kutafuta haki kwa waathiriwa wa uhalifu wa kivita.
Liz Evenson kutoka Human Rights Watch alisema, "vikwazo hivi vitawanyima waathiriwa fursa ya kupata haki.”
Vikwazo vilivyolenga Mwendesha Mashtaka Mkuu
Agizo la Februari kutoka kwa Rais Trump linamzuia Khan na wafanyakazi wengine wasio Wamarekani wa ICC kuingia Marekani. Pia, agizo hilo linatishia faini na kifungo kwa yeyote atakayempa Khan msaada wa kifedha, vifaa au kiteknolojia.
Hali hiyo imeathiri si uchunguzi dhidi ya viongozi wa Israel tu, bali pia kesi nyingine muhimu kama ya Sudan dhidi ya rais wa zamani Omar al-Bashir aliyeshtakiwa kwa mauaji ya halaiki. Uchunguzi huo sasa umesimama licha ya ripoti za uhalifu mpya.
Wakili Eric Iverson, anayehusika na kesi ya Sudan, amefungua kesi dhidi ya serikali ya Marekani akitaka ulinzi dhidi ya vikwazo. Wakili wake Allison Miller alisema Iverson hawezi hata kutekeleza majukumu ya kawaida ya mawakili.
Soma pia: Netanyahu ziarani nchini Hungary akaidi amri ya ICC
Wamarekani wanaofanya kazi ICC wameonywa kuwa huenda wakakamatwa wakirejea nyumbani, na tayari maafisa sita wa ngazi ya juu wameondoka mahakamani kwa hofu ya vikwazo.
Mahakama yatelekezwa na washirika wake
Mahakama hiyo hutegemea kwa kiasi kikubwa mashirika ya kiraia na wakandarasi, lakini baadhi yao wamesitisha shughuli kutokana na hofu ya kulengwa na mamlaka za Marekani. Kampuni ya Microsoft ilifuta barua pepe ya Khan, na akaunti zake za benki nchini Uingereza zimefungwa.
Mashirika yanayosaidia kukusanya ushahidi na mashahidi yamehamisha fedha zao kutoka benki za Marekani kwa hofu ya kuzuwiliwa pesa zao. Mashirika mengine mawili makubwa ya haki za binadamu yamesitisha ushirikiano na ICC, wafanyakazi wao wakiepuka hata kujibu barua pepe kutoka kwa maafisa wa mahakama.
Maafisa wa ICC walioomba majina yao yasitajwe wanasema kuna hofu kuwa taasisi hiyo haitavuka kipindi cha Trump. Mmoja wao alisema, "Sijui kama tutadumu kwa miaka minne ijayo.”
Trump aituhumu ICC kwa upendeleo na hatari kwa usalama wa taifa
Trump alitoa vikwazo muda mfupi baada ya ICC kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahuna aliyekuwa waziri wa ulinzi Yoav Gallant kwa tuhuma za uhalifu wa vita dhidi ya raia wa Gaza. Israel imekanusha madai hayo.
Trump aliituhumu ICC kwa kuchukua hatua "batili na zisizo halali” dhidi ya Marekani na mshirika wake wa karibu Israel. Alisema ICC inaleta hatari kwa wanajeshi wa Marekani na kuvuruga sera zake za nje na usalama wa taifa.
Soma pia:Umoja wa Mataifa wamtaka Trump abadilishe uamuzi wa kuiwekea vikwazo ICC
Netanyahu aliziita tuhuma hizo za ICC kuwa "za kipuuzi,” na bunge la Israel linaandaa mswada wa kuzuia utoaji wa ushahidi kwa ICC kama kosa la jinai.
Mizaha ya Giza, tuhuma mpya dhidi ya Khan, na kesi za awali
Ndani ya ICC, baadhi ya wafanyakazi wanaendelea kwa ucheshi wa giza, wakitania kuwa hata kumpa Khan kalamu kunaweza kuwagharimu.
Hii si mara ya kwanza Trump anailenga ICC. Mwaka 2020, serikali yake iliwalenga Fatou Bensouda na msaidizi wake kwa uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita Afghanistan. Rais Biden aliondoa vikwazo hivyo alipoingia madarakani.
Kesi tatu za kisheria bado zinaendelea dhidi ya serikali ya Trump, kutoka kwa wafanyakazi na washauri wa ICC nchini Marekani, wakidai vikwazo vinakiuka uhuru wa kujieleza. Iverson alipata ulinzi wa muda, lakini Wamarekani wengine ICC hawajapata kinga kama hiyo.
Mahakama pia imekumbwa na ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya mataifa wanachama. Nchi tatu, mbili zikiwa wanachama wa Umoja wa Ulaya, zimekataa kutekeleza hati za kukamatwa za ICC.
Katika miezi ya hivi karibuni, majaji wamemzuia Khan kuchapisha maombi ya hati za kukamatwa katika baadhi ya uchunguzi, ikiwemo ule wa Afghanistan na Ukingo wa Gaza.
Zaidi ya hayo, Khan anatuhumiwa na wafanyakazi wawili wa ICC kwa unyanyasaji wa kingono dhidi ya msaidizi wake wa kike, madai anayoyakana vikali. Umoja wa Mataifa unaendesha uchunguzi, huku Khan akituhumiwa pia kuwakandamiza waliomuunga mkono mlalamikaji.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu sasa inakabiliana na changamoto kubwa zaidi kuwahi kuikumba, huku mustakabali wake ukiwa mashakani katikati ya vikwazo vya kisiasa, tuhuma za ndani, na hali ya kutoaminiana kutoka kwa washirika wa kimataifa.