Syria yasema vikosi vyake vinajiondoa mjini Sweida
17 Julai 2025Marekani ambayo ni mshirika wa karibu wa Israel na ambayo imeanza kufufua uhusiano wake na Syria, ilisema kwamba makubaliano yamefikiwa ya kurejesha utulivu katika eneo hilo la Sweida na kuzihimiza "pande zote kuheshimu ahadi walizotoa".
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio aliandika kupitia mtandao wa X akisema kuna mafanikio katika kukomesha mapigano kusini mwa Syria yaliyozuka mwishoni mwa juma na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300.
Waziri huyo alisema kuwa wamezishirikisha "pande zote zinazohusika katika mapigano nchini Syria," na kukubaliana juu ya hatua mahususi ambazo zitamaliza hali hiyo ya kutatanisha na ya kutisha usiku wa jumatano bila kutoa maelezo zaidi.
Hapo awali serikali ya Syria ilikuwa imetangazamakubaliano mapya ya usitishaji mapigano huko Sweidaambayo yangesimamisha operesheni za kijeshi, baada ya makabiliano makali tangu siku ya Jumapili. Taarifa iliyotolewa na wizara ya ulinzi ya Syria ilisema kuwa jeshi lake "limeanza kujiondoa kutoka mji wa Sweida katika utekelezaji wa masharti ya makubaliano yaliyopitishwa baada ya kumalizika kwa operesheni ya kupambana na vikundi haramu" kwenye mji huo.
Taarifa hiyo hata hivyo haikutaja kuondolewa kwa vikosi vingine vya usalama vya serikali, ambavyo vilitumwa mjini humo siku ya Jumanne kwa lengo la kusimamia makubaliano ya awali yaliyofikiwa na viongozi wa jamii ya Druze kufuatia siku kadhaa za mapigano makali na makabila ya Bedui.
Usitishaji huo wa mapigano ulionekana kutofanikiwa huku mashahidi wakiripoti kwamba vikosi vya serikali viliungana na jamii ya Bedui katika kushambulia wapiganaji wa Druze na raia.
Kabla ya kutangazwa taarifa za kujiondoa kwa vikosi vya serikali ya Syria mjini Sweida, Israel ilifanya mashambulizi makali ya anga mjini Damascus siku ya Jumatano na kulipua sehemu ya wizara ya ulinzi na kupiga karibu na ikulu ya rais huku ikiapa kuharibu vikosi vya serikali vinavyoshambulia Druze kusini mwa Syria na kuwataka waondoke.
Mashambulizi hayo yaliashiria ongezeko kubwa la uhasama wa Israel dhidi ya utawala unaoongozwa na Rais wa mpito Ahmed al-Sharaa. Ikiwaelezea watawala wapya wa Syria kama wanasiasa wenye misimamo mikali wasiojificha, Israel iliapa kuilinda jamii ya Druze dhidi ya mashambulizi, ikisukumwa na wito kutoka kwa Waisraeli walio wachache wa Druze.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana leo Alhamisi kushughulikia mzozo huo.