Marsabit na juhudi za kutunza utamaduni wa jamii za wafugaji
23 Mei 2025Kizazi cha leo kinashindwa kuendeleza mila na desturi zao za jadi na badala yake kugeukia mila za kuigwa kutoka mataifa ya kigeni. Hali hii imewachochea vijana kutoka kwenye jimbo la Marsabit, Kenya kuanzisha makavazi na maktaba ya kuhifadhi sanaa na utamaduni, ili kuuelimisha ulimwengu kuhusu utamaduni wa wafugaji kutoka jimboni humo.
Kutokana na mila na desturi ya jamii nyingi Kenya kuanza kudidimia, haja ya kuhifadhi na kuambatanisha utamaduni na teknolojia ya kisasa pamoja na kukuza sekta ya utalii humu nchini, imeanza kushika kasi miongoni mwa vijana jimboni Marsabit.
Makavazi kwa ajili ya kuielimisha jamii kuhusu utamaduni
Kundi la vijana wanaojiita Marsabit Botanical Garden limeanzisha makavazi na linanuia kuyatumia kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vya kitamaduni pamoja na kuielimisha jamii kuhusu utamaduni wao wa jadi kupitia mfumo wa kidijitali. Galgallo Roba Guyo, mkurugezi wa kundi hilo, anasema makavazi hayo pia yanatumika kama maktaba ya vitabu vya lugha asili na tamaduni za jamii zote zinazoishi katika ukanda huo wa kaskazini mwa Kenya.
''Tumekuwa na kongomano la vijana wenye uelewa wa masuala ya kitamaduni kutoka hapa Marsabit. Tukiangalia jamii asilia, wanaendelea kupoteza utamaduni wao wa kale ikiwemo lugha,'' alibainisha Guyo. Anasema walichochewa sana kuanzisha mchakato wa kuhifadhi utamaduni wa makabila na jamii tofauti jimboni hapa, baada ya kubainika kuwa baadhi ya jamii zilikuwa zinakabiliwa na hatari ya kupoteza utamaduni wao na lugha yao asili.
Hofu ya baadhi ya utamaduni wa jamii nchini kupotea ni suala ambalo wanachama wa kikundi cha Marsabit Botanical Garden wanalihofia. Sora Halake Sora ni mwanachama wa kundi hilo na anasema, ''masuala ya utamaduni kwa wakati huu yanadidimia ikilinganishwa na hapo nyuma. Kulikuwa na utamaduni wa kuangalia hali ya hewa, lakini kwa sasa watu wengi hawatambui hilo.''
Idadi kubwa ya wazee wa leo hawana ufahamu na uelewa wa mila zao, hivyo kuchangia vijana kusalia gizani kuhusu desturi zao za jadi. Kulingana na David Latao kutoka eneo la Karare, wazee wa karne hii hawawezi kuwaelimisha vijana kuhusu tamaduni zao na hivyo kuchangia kudidimia kwa mila kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Wazee wanaweza kuwasaidia vijana
''Mimi nimetoka ukoo wa Milakomono, lakini kuna vitu kadhaa ambavyo sielewi, japo wazee na watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea ndiyo wanaelewa. Wao ndio wanaweza kutusaidia kuelewa vitu vya kuhifadhi ili mila zetu zisipotee,'' alifafanua Lato.
Mtaalamu wa masuala ya utamaduni Dokta Evans Taracha ametaja uoga kutoka kwa wazee kuwa ndiyo unachangia mila nyingi kuendelea kudidimia, kwani wazee hao hawana ujuzi wa nanma ya kuwafundisha vijana wadogo kuhusu mila zao. ''Changamoto kuu ni kwamba, wenye maarifa hususan wazee hawana imani maarifa yao yanaweza kuisaidia jamii na wao wenyewe. Tunaendelea kuwahamasisha kuhusu hilo,'' alifafanua Dokta Taracha.
Hatua ya vijana kuanza kukumbatia mila zao na kuzinduwa makavazi na maktaba ya kutunza mila hizo kidijitali inatafsiriwa kama itakayokuwa na mwamko mpya kwa jamii zinazoishi kaskazini mwa Kenya na huenda ikachangia uwiano miongoni mwa kizazi kijacho.
Naibu Gavana wa Kaunti ya Marsabiti, Solomon Riwe, anasema serikali yake iko tayari kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuutekeleza mradi huo. ''Katika mpango wetu wa maendeleo, tunataka bunge lipitishe fedha za ziada tutakazoziomba kwa ajili ya masuala ya maendeleo kama haya kwa faida ya jamii zetu,'' alisisitiza Riwe.
Katika kuweka siri taarifa na maarifa yanayonakiliwa kwa jamii kabla ya kuchapishwa rasmi kwenye mfumo wa kitaifa, vijana ambao wanahusika na ukusanyaji wa taarifa hizo huwa wanaapa kutekeleza majukumu yao na kuweka siri taarifa watakazokuwa wananakili. Kupitia mikakati hiyo, idara ya utamaduni ya kaunti ya Marsabit imeelezea matumani makubwa ya kupiga jeki uhifadhi wa utamaduni na uzalishaji wa mapato kutokana na utamaduni wa jamii asili zinazoishi Marsabit.
Mtayarishaji wa makala hii ni Miachel Kwena