Vijana waanza kurekodi vitendo vya uhalifu Goma
23 Julai 2025Tangu mwezi Januari mwaka huu, mji wa Goma na maeneo mengine mengi ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yako mikononi mwa waasi wa AFC/M23. Katika ripoti yake iliyochapishwa mapema mwezi huu wa Julai, kundi hilo la vijana limeorodhesha jumla ya visa 47 vya mauaji, visa 75 vya ubakaji, watu 14 waliotekwa na matukio 66 ya uporaji, vyote hivi katika kipindi cha mwezi mmoja.
Kama anavyofafanua Jules Ngeleza, mmoja wa vijana wanaounda kundi hilo la kujitolea na aliyechangia katika kuandaa ripoti hiyo, madhumuni ya kundi lao ni kuhakikisha kuwa wanaofanya uhalifu huo watafikishwa mbele ya sheria siku za usoni.
Mwakilishi wa UN azuru mashariki mwa Kongo, hali ingali tete
"Lengo la mpango huu ni kuweka kumbukumbu na kuchapisha matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, ili kuhimiza kurejeshwa kwa amani. Pia ni kazi ya kumbukumbu na haki, ili siku moja wahusika wa uhalifu huu wawajibishwe.''
Kwa mujibu wa Jules Ngeleza, hali inaendelea kuwa mbaya zaidi mjini Goma na katika maeneo jirani. Tangu kuchapishwa kwa ripoti hiyo mwanzoni mwa Julai, watu wengine wasiopungua 13 wameuawa, kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na kikundi hicho cha uchunguzi. Aidha, visa vingine 25 vya ubakaji vimeripotiwa, hasa katika miji ya Goma, Sake na Rutshuru, kwa mujibu wa vyanzo vya kitabibu vya eneo hilo ambavyo havikutaka kutajwa majina.
Baadhi ya wakaazi wa Goma, kama msichana huyu ambaye pia aliomba kutotambulishwa kwa jina, wanasimulia hali yao ya kukata tamaa.
Waasi wa M23 waendelea kuajiri vijana wapiganaji mjini Goma
"Mbali na waliouawa wakati M23 walipoukamata mji wa Goma, tangu walipochukua udhibiti, nimeona watu wawili kutoka mtaa wetu wakiuawa. Siku iliyofuata walikuja vijana wakaanza kuuliza maswali. Tunahitaji amani, tumechoka.”
Asasi za kiraia za Kivu Kaskazini zina wasiwasi kuhusu ukimya wa serikali katika kuwatetea wakaazi wa eneo hilo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mwanachama wa mojawapo ya asasi hizo, Justin Murutsi, anasema wanajihisi kama wametelekezwa.
"Serikali ina jukumu la kulinda usalama wa raia. Lakini kunapokuwa na mauaji kama haya na hakuna tamko lolote kutoka kwa watawala, hilo linaonyesha pengo kubwa la kiuongozi.”
Bunge la Kongo lajadili mzozo wa mashariki mwa nchi
Ni pengo hilo ambalo kundi hili la vijana wa Goma linajaribu kuliziba kwa kuorodhesha idadi ya waathirika waliorekodiwa mjini humo na maeneo ya jirani. Kufuatia tuhuma hizi, viongozi wa AFC-M23 wanasema baadhi ya mauaji hayo ni ya ulipizaji kisasi unaofanywa na watu binafsi, hasa yale yanayowalenga wafanyabiashara ya ubadilishaji wa fedha.
Benjamin Mbonimpa, Katibu Mkuu wa muungano wa waasi wa AFC-M23, anasema hatua zimechukuliwa, kama vile doria zilizoongezwa na kuweka kamera za usalama za zinazoweza kufanya kazi gizani, katika mitaa kadhaa ya Goma.
Chanzo: Ripoti ya Yvonne Kapinga/DW Goma