Video ya Macron akipigwa na mkewe yazua gumzo mtandaoni
26 Mei 2025Katika video hiyo, mkono wa Brigitte – ambao ndiyo sehemu pekee ya mwili wake iliyokuwa ikionekana – ulitua usoni mwa Macron, ambaye aligeuka kumtazama mkewe, kisha akaangalia kamera na kuwapungia mkono waliokuwa wamekusanyika kumpokea.
Kwa mujibu wa watu wa karibu na rais, tukio hilo lilikuwa sehemu ya masihala kati ya wanandoa hao kabla ya kuanza rasmi kwa ziara hiyo ya kitaifa.
"Ilikuwa ni wakati wa kupumzika kidogo na kufurahia kabla ya shughuli rasmi kuanza,” chanzo kimoja kililiambia shirika la habari la dpa.
Hata hivyo, kabla ya maelezo hayo rasmi kutolewa, tayari tetesi zilikuwa zimezagaa mtandaoni kwamba Brigitte alimpiga mumewe kwa nguvu.
"Hilo tu liliwatosha waumini wa nadharia za njama kupata jambo la kulizungumzia,” alisema mtu wa karibu na rais.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa televisheni ya serikali ya Urusi, RT (Russia Today), hapo awali ilishawahi kudokeza kuwa Rais Macron huwa anapigwa na mkewe – tuhuma ambazo zimewahi kuibuliwa mara kadhaa na vyombo vya Urusi.
Kwa sasa, mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na nchi nyingine kadhaa tayari yamefuta leseni ya kurusha matangazo ya RT, katika jitihada za kudhibiti ueneaji wa propaganda za vita kutoka Urusi na taarifa potofu.
Tuhuma za awali zakanushwa na Ikulu ya Élysée
Katika tukio lingine la upotoshaji, Ikulu ya Élysée ilikanusha vikali ripoti ya uongo kuhusu mfuko uliodaiwa kuwa na dawa za kulevya aina ya kokaini ambao ulidaiwa kumilikiwa na Macron alipokuwa safarini kuelekea Kiev kwa treni.
Uvumi huo ulisambazwa na tovuti inayofanana na zile zilizotajwa na serikali ya Ufaransa kuwa sehemu ya mtandao wa upotoshaji wa Urusi.
Kwa sasa, Rais Macron na mkewe wanaendelea na ziara ya kiserikali katika nchi za Vietnam, Indonesia, na Singapore, ambayo inatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa.
Katika ziara hiyo, Macron anatarajiwa kujadili masuala ya ulinzi na changamoto za mazingira na viongozi wa mataifa hayo.