Venezuela yawaachia Wamarekani sita kufuatia mazungumzo
1 Februari 2025Wamarekani sita waliozuwiliwa nchini Venezuela katika miezi ya karibuni wameachiwa na serikali ya Rais Nicolas Maduro, baada ya kukutana Ijumaa na afisa wa utawala wa Trump aliepewa jukumu la kumhimiza kiongozi huyo kukubali kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa nchini Marekani.
Rais Donald Trump na mjumbe wake wa majukumu maalumu Richard Grenell, wametangaza kuachiliwa kwa wanaume sita kupitia mitandao ya kijamii.
Ziara ya Grenell nchini Venezuela ilikuja kama mshangao kwa Wavenezuela wengi, waliotumaini kwamba Trump angeendeleza kampeni ya shinikizo kubwa aliyoiendesha dhidi ya Maduro katika muhula wake wa kwanza.
Soma pia: Nchi za magharibi za kosoa vikali kuapishwa kwa Maduro
Televisheni ya taifa ya Venezuela iliyonyesha picha za Grenell na Maduro wakizungumza katika kasri la Rais, na kusema mkutano huo uliombwa na serikali ya Marekani.
Serikali ya Marekani, sawia na mataifa mengine ya magharibi, haitambui ushindi wa Maduro katika uchaguzi wa mwaka jana na badala yake ilitangaza kumtambua mgombea wa upinzani, Edmundo Gonzalez Urrutia kama mshindi halali wa kinyang'anyiro hicho.