VATIKAN CITY: Papa kujitokeza kwa ufupi kwa baraka za Pasaka
27 Machi 2005Papa John Paul wa pili anatazamiwa kujitokeza kwa muda mfupi leo hii Jumapili ya Pasaka kuwapa baraka zake waumini lakini siku hii ya furaha kubwa katika kalenda ya Wakristo itakuwa na kidowa kidogo cha huzuni na hali ya mashaka kutokana na kudhoofika kwa afya yake.
Papa mwenye umri wa miaka 84 amekasimu misa hiyo kufanywa kwa niaba yake na kadinali mwandamizi kama alivyofanya kwa sherehe zote za msimu wa Pasaka ambazo zimeanza wiki moja iliopita.
Muda wa kushiriki kwa Papa katika Pasaka ya Jumapili leo asubuhi unatazamiwa kupunguzwa mno ili kumuwezesha kutunza nguvu zake na kuendelea kupata nafuu kutokana na operesheni ya koo aliyofanyiwa hapo Februari 24 ili kumpunguzia matatizo ya kupumuwa.
Misa ya Jumapili ya Pasaka katika Uwanja wa St.Peter itaongozwa na Kadinali Angelo Sodano ambaye ni mkuu wa masuala ya kigeni wa Papa John Paul.