VATICAN. Papa Yohana Paulo wa Pili yu hali mahututi.
1 Aprili 2005Makao makuu ya kanisa katoliki, Vatican yametangaza kwamba hali ya afya ya kiongozi wa kanisa hilo, baba mtakatifu Yohana Paulo wa Pili, inaendelea kuwa mbaya. Msemaji wa Vatican, Joaquin Navarro-Valls, amesema kiongozi huyo aliombewa maombi maalumu ya watu wanaokaribia kuaga dunia ya Viaticum mapema leo. Habari kwamba baba mtakatifu amepotelewa na fahamu zake, zimekanushwa na maafisa wa Vatican. Hata hivyo, inasemekana hali yake imefikia pabaya. Tangazo hilo la Vatican limeeleza pia kuwa baba mtakatifu alisaidiwa kupumua hapo jana na leo asubuhi. Maafisa wanasema aliamua mwenyewe asipelekwe hospitalini. Hali yake ya afya ilianza kuwa mbaya hapo jana wakati kiwango chake cha joto mwilini kilipopanda kufuatia homa kali. Kwa mujibu wa Vatican, baba mtakatifu alipatwa na mshutuko wa moyo hapo jana. Wakati huo huo, waumini na wafuasi wa dini walikusanyika katika kiwanja cha St Peters mjini Rome kumuombea kiongozi huyo.