VATICAN: Papa atakiwa aombe msamaha
15 Septemba 2006Viongozi wa kiislamu wanamtaka kiongozi wa kanisa Katoliki papa Benedict wa 16 aombe msamaha kwa matamshi yake kuhusu uislamu wakati wa ziara yake hapa Ujerumani.
Kiongozi wa baraza la waislamu nchini Misri amezitaka nchi za kiislamu zitishie kukatiza mahusiano na makao makuu ya kanisa Katoliki huko Vatican mpaka Baba Mtakatifu afutilie mbali matamshi yake.
Kumezuka hasira miongoni mwa waislamu duniani kote hii leo. Nchini India kiongozi wa waislamu amesema papa Benedict wa 16 amekuwa kama mhubiri wa karne ya 14.
Mjini Gaza guruneti limelipuka nje ya kanisa moja ingawa hakuna uharibifu uliotokea wala watu waliojeruhiwa.
Waziri mkuu wa Palestina, Ismail Haniyah, ameyalaani vikali matamshi ya papa na amemtaka awache kuuingilia uislamu.
Na huko nchini Lebanon, shehe mkuu wa Washia, Sheikh Mohammed Hussein Fadlallah, leo amemkosoa papa Benedict wa 16 kwa kuulinganisha uislamu na machafuko.