VATICAN-Papa ashindwa kuongoza misa ya Jumapili ya Pasaka kwa mara ya kwanza tangu awe Papa.
27 Machi 2005Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili leo alitoa mibaraka kwa maelfu ya waumini waliokuwa wamekusanyika nje ya uwanja wa kanisa la Mtakatifu Pita,lakini hata hivyo alishindwa kuongea.Baba Mtakatifu mwenye umri wa miaka 84 alijitokeza dirishani kwake baada ya mmoja wa Makadinali wake kuendesha misa wa Pasaka.
Baba Mtakatifu alikaa dirishani hapo wakati Kadinali Angelo Sodano,alipokuwa akisoma ujumbe wa Pasaka kwa Roma na kwenda sehemu zote duniani,ujumbe ambao ulisisitiza amani katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika na kuwepo mshikamano wa ukarimu kwa maelfu ya watu wanaokufa kutokana na umasikini pamoja na njaa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Yohanne Paulo wa pili katika kipindi cha miaka 26 ya kuwa Papa,kutoongoza misa ya Jumapili ya Pasaka.Mara ya mwisho alipomudu kuzungumza mbele ya umati wa watu,ni wiki mbili zilizopita,siku ambayo alitolewa hospitalini baada ya kupata ahueni kutokana na operesheni ya koo ya kumuondolea matatizo ya kupumua.