VATICAN. Maelfu ya waombolezaji watoa heshima zao kwa marehemu Yohana Paulo wa Pili.
5 Aprili 2005Maelfu ya waombolezaji wanaendelea kutiririka kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu baba mkatatifu Yohana Paulo wa pili katika kanisa la mtakatifu Petro. Kanisa hilo litakuwa wazi kwa muda wa saa tatu kila siku, kuwaruhusu maelfu ya watu waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu hadi mjini Rome, kutoa heshima zao za mwisho. Mazishi ya marehemu yatafanyika siku ya Ijumaa ijayo mwendo wa saa nne asubuhi saa za Itali, katika sherehe ya hadhara. Viongozi wasiopungua 200 kutoka ulimwenguni kote wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo. Papa Yohana Paulo wa pili atazikwa katika kanisa la Mtakatifu Petro, na wala sio kwao Poland, ili kuendeleza desturi ya Vatican. Hapo awali kulikuwa na tetesi kwamba kiongozi huyo angesitiriwa mjini Krakow, Poland. Misa ya wafu itasomwa na kadinali wa Ujerumani, Joseph Ratziger. Wakati huo huo, Vatican huenda ikakatiza uhusiano wake na Taiwan na kuitambua China, iwapo Beijing itaahidi kuzingatia uhuru wa kidini.