VATICAN. Kadinali wa kijerumani achaguliwa papa mpya wa kanisa Katoliki.
20 Aprili 2005Kuchaguliwa kwa papa Benedict wa 16 kuliongoza kanisa katoliki, ambaye kufikia jana jioni aliitwa kadinali Joseph Ratzinger, kumepokelewa kwa furaha isiyo kifani na viongozi wa Ujerumani.
Kansela Gerhard Schroeder amesema ni heshima kubwa kwa Ujerumani, huku akimsifu kiongozi huyo kwa kusema alistahili kulijaza pengo lililowachwa na marehemu Yohana Paulo wa pili. Amesema ni kiongozi anayelifahamu zaidi kanisa ulimwenguni kote, na ni mwanatheolojia anayejulikana duniani.
Rais Horst Köehler amemtakia papa Benedict wa 16 ujasiri na nguvu katika utendaji wake. Amesema kuchaguliwa kwa Ratzinger kumewafurahisha wajerumani na ni jambo la kujivunia.
Rais wa Marekani, George W Bush amemtaja papa mpya kuwa mtu mwenye hekima kubwa na maarifa, na anayemtumikia Mungu.
Waziri mkuu wa Uingereza bwana Tony Blair, kupitia msemaji wake, amempongeza papa na kumtakia kila la heri katika kazi yake. Ameelezea matumaini yake ya kuendelea kuwepo ushirikiano kati ya Uingereza na Vatican kuhusu maswala yenye umuhimu wa kimataifa kama vile bara la Afrika na maendeleo.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Kofi Annan, amesema papa Benedict wa 16 ana ujuzi mwingi na anatumai ataweza kuchangia pakubwa katika maisha ya kiroho ya waumini kama alivyofanya marehemu Yohana Paulo wa pili.
Naye rais wa Ufaransa, Jacques Chirac, amemtakia papa mpya kila la heri na kuahidi kwamba Itali itaendelea kufuatilia mazungumzo ambayo imekuwa nayo na Vatican, ya kutetea amani, haki, mshikamano na hadhi ya binadamu.
Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, kwa upande wake amempongeza papa na kumtakia ufanisi. Anatumai uhusiano kati ya Palestina na Vatican utaendelea kuimarika na kwamba Vatican itaendelea kutetea haki ya kweli katika taifa hilo takatifu.
China imemtaka papa Benedict wa 16 kukatiza uhusiano na Taiwan na ajiepushe mbali na mswala ya ndani ya China ili kuboresha uhusiano kati ya China na Vatican.