VATICAN CITY : Shinikizo didi ya papa lapamba moto
17 Septemba 2006Papa leo hii anatarajiwa kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tokea kuibuka kwa hasira ya Waislamu kutokana na matamshi aliyoyatowa juu ya Uislamu huku shinikizo likiongezeka kumtaka aombe radhi binafsi.
Makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatikani ilitowa taarifa hapo jana ikisema kwamba Papa alikuwa anasikitika sana kwamba Waislamu wamekasirishwa na hotuba yake ambayo maana yake imeeleweka vibaya lakini mataifa ya Kiislam na makundi ya Kiislam yamendelea kuelezea hasira zao kwa matamshi ambayo wanahisi yameuelezea Uislamu kama dini yenye dosari ya matumizi ya nguvu.
Papa Benedikt wa 16 kiongozi wa Wakristo wa madhehebu ya Katoliki milioni 1. 1 duniani leo anatazamiwa kutowa mahubiri yake ya kawaida ya kila Jumapili yanayojulikana kama Angelus katika kanisa la St.Peter sala ambayo mara nyingi hutumiwa na papa kuelezea maoni ya kanisa juu ya matukio makuu duniani.
Mgogoro huo wa kwanza kumkumba Papa Benedikt tokea ashike wadhifa huo miezi 17 iliopita umechochewa na hotuba yake hapo Jumanne nchini Ujerumani akigusia shutuma zilizotolewa dhidi ya Mtume Muhammad SAW na Mfalme wa Kikristo wa Karne ya 14 kwamba alichokileta kiongozi huyo wa Waislamu ilikuwa ni uovu tu mathlan kwa kueneza dini aliyokuwa akihubiri kwa kutumia upanga.
Morocco na Misri zimewarudisha mabalozi wao nyumbani waliokuwa Vatikan na chama cha Ndugu wa Kiislam nchini Misri Muslim Brotherhood kimesema kuomba radhi huko hakutoshi na kwamba Benedikt amefanya makosa na lazima alitambuwe hilo.
Ziara ya Papa iliopangwa kufanyika nchini Uturuki hapo mwezi wa Novemba imeingia mashakani kufuatia matamshi hayo.Waziri Mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema matamshi hayo ya Papa ni mabaya na ya bahati mbaya kwamba yanapaswa kutenguliwa na Rais wa Yemen Ali Abdallah Saleh amemshutumu hadharani papa kwa matamshi yake hayo.
Watu walioko ndani ya makao makuu ya Vatikan na wanadiplomasia wanasema Papa yumkini akawa amechanganya dhima yake mpya na nyadhifa zake za zamani kama mwanataaluma wa elimu ya dini katika Kanisa Katoliki.