VATICAN CITY : Papa asoma hotuba kamili baada ya kuumwa
20 Februari 2005Katika sauti iliopwelea lakini yenye nguvu kwa wastani Papa John Paul wa Pili amesoma hotuba yake kamili ya kila wiki leo hii kwa mara ya kwanza tokea alipotibiwa hospitalini mapema mwezi huu kwa matatizo ya kupumuwa.
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita Papa mwenye umri wa miaka 84 ameweza tu kutowa baraka zake kwa ufupi kwa kunon’gona mwisho wa sala ya Bikira Maria na kumwachia msaidizi wake asome hotuba refu.
Katika kile kinachonekana kuwa anapata nafuu Papa alisoma ujumbe kamili na kuuambia umma uliokuwepo katika uwanja wa St.Peter kwamba kazi muhimu ya upapa ni kuhakikisha umoja wa Kanisa na kuongeza kwamba wito wa kuulinda umati wake wa waumini wa Kikristo hususan uko uhai kwenye nafsi yake.
Wahakiki wa masuala ya Vatican wanasema kauli hiyo ni dokezo kwamba Papa ameazimia kuendelea kuwa kiongozi wa Wakristo wa madhehebu ya Katoliki bilioni 1. 1 na hana nia ya kujiuzulu.