VATICAN CITY : Maelfu wakesha kumuombea Papa aliye mahtuti
2 Aprili 2005Uwanja wa St Peter katika makao makuu ya kanisa Katoliki huko Vatikan nchini Italia ulikuwa umefurika takriban watu 70,000 katika mkesha wa ibada ya usiku kucha kumuombea Papa John Paul wa Pili ambaye yuko mahtuti na wengine zaidi wamekuwa wakiwasili alfajiri hii.
Kwa mujibu wa polisi waumini kati ya 50,000 na 70,000 walikuwako katika uwanja huo mkubwa kabisa macho yao yakiwa yameelekezwa kwenye nyumba ya papa iliokuwa ikiwaka taa.
Idadi hiyo ya waumini imekuwa ikiongezeka kwa dakika kujiunga na sala ya maombi kumuombea Papa huyo mwenye umri wa miaka 84.
Usiku wa manane Padre Angelo Comastri mwakilishi mkuu wa papa katika Mji wa Vatican aliwaandaa mahujaji kwa ajili ya dakika za mwisho za uhai wa Papa kwa kuwaongoza katika sala ya rozari.
Amesema jioni hii au usiku huu Yesu Kristo anamfungulia mlango Papa.
Hali ya Papa imeelezwa kuwa mbaya sana baada viungo vyake muhimu kushindwa kufanya kazi.Pumzi zake zimezidi kupunguwa na shinikizo lake la damu limeshuka mno kufikia kiwango cha hatari. Hata hivyo Vatican imekanusha repoti kwamba moyo na ubongo wake vimesita kufanya kazi.
Kufuatia wiki kadhaa za kuzorota kwa afya yake Papa alipata homa kali hapo Alhamisi iliosababishwa na maambukizi kwenye mkojo wake.
Waumini wa kanisa Katoliki wamekuwa wakikusanyika makanisani duniani kote kumuombea Papa.Mojawapo ya mkusanyiko mkubwa ulikuwa kwenye Kanisa la Cologne hapa Ujerumani ambapo waumini wamekuwa pia katika mkesha wa ibada.