VATICAN CITY : Kanisa kujadili masuala yatakayomkabili Papa mpya
9 Aprili 2005Kanisa Katoliki la Rome linaanza katika kipindi cha siku tisa zijazo kujadili masuala mengi ambayo yumkini yakamkabili mrithi wa Baba Mtakatifu Yohana Paul wa Pili baada ya kutowa heshima zake za mwisho katika Misa adhimu ya mazishi hapo jana.
Makadinali 117 wanaotarajiwa kumchaguwa papa mpya katika baraza la siri kuanzia tarehe 18 mwezi wa April watakuwa wanakutana kila siku katika vikao vya faragha vya awali huko Vatican na kwenye mikahawa ya Rome kubadilishana mawazo juu ya namna ya kuwongoza waumini wa madhehebu ya Katoliki bilioni moja na milioni moja duniani.
Zaidi ya makadinali 160 wa Kanisa hilo ikiwa ni pamoja na wale waliopindukia umri wa miaka 80 ambao hawawezi tena kupiga kura waliungana na watu wenye hadhi kubwa pamoja na maskini katika mazishi ya Vatican hapo jana kwa mwananchi huyo wa Poland aliyeliashiria Kanisa duniani kote katika kipindi chake cha kuliongoza cha miaka 26.
Wakati makadinali kadhaa wamesema kabla ya maziko hayo kwamba walikuwa wakimtaka papa mwengine kama John Paul wa Pili wanajuwa kwamba hana mtu anayeeleweka kumrithi.Wataliana na Waamerika Kusini kadhaa wamewekewa matumaini ya kuchaguliwa lakini mabaraza hayo ya siri ya kumchaguwa papa chaguo lao linaweza na huwa la kushangaza.
Zaidi ya viongozi 200 wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa duniani na viongozi wa kidini pamoja na mamia na maelfu ya waombolezaji walifurika kwenye uwanja wa St. Peter hapo jana kwa mazishi ya Papa ambaye mwili wake umezikwa kwenye chumba cha chini ya Kanisa la St.Peter mjini Rome.