VATICAN CITY : Baba Benedikt atawazwa kuwa Papa
24 Aprili 2005Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 ametawazwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani leo hii kwa kupokea nembo za ishara ya mamlaka yake katika Misa ya wazi kwenye uwanja wa St.Peter mjini Rome Italia ambayo imechanganyisha pamoja sherehe za mtindo wa kale na sala.
Wakati wa kuanza mahubiri yake ya kutawazwa Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 amesema Kanisa linashikilia mustakbali wa dunia mikononi mwake.
Amewaambia viongozi wa dunia na mamia ya maelfu ya watu waliofurika uwanja wa St.Peter kwamba kanisa linashikilia mustakbali wa dunia na kwa hiyo linamuonyesha njia kila mmoja wao kuelekea kipindi hicho cha usoni.
Benedikt wa 16 aliechaguliwa hapo Jumanne kuwa Papa wa 265 wa Kanisa Katoliki amesema hiyo ni kazi kubwa ambayo kwa kweli inapindukia uwezo wote ule wa binaadamu.
Ameongeza kusema hayuko peke yake na kwa msaada wa Mungu haitoibeba kazi hiyo pekee kwani kwa kweli amesema asingeliweza katu kuibeba kazi hiyo peke yake.