VATICAN: Baba mtakatifu kuzikwa siku ya Ijumaa.
4 Aprili 2005Makadinali wa kikatoliki kutoka sehemu mbali mbali duniani wako mjini Roma kukamilisha shughuli ya mazishi ya baba mtakatifu Yohana Paulo wa pili aliyefariki dunia siku ya jumamosi baada ya kuugua.
Makadinali hao baada ya kusoma ridhaa ya baba mtakatifu Yohana Paulo wa pili kuhusu lini na mahala atakapozikwa wametangaza kuwa baba mtakatifu atazikwa siku ya Ijumaa.
Baada ya mazishi makadinali watamchagua mrithi atakae liongoza kanisa katoliki.
Habari kutoka Vatican zinaeleza kuwa maelfu ya waombolezaji wanatiririka katika mlolongo mkubwa ili kutoa heshima zao za mwisho kwa baba mtakatifu Yohana Paulo wa pili katika kanisa la mtakatifu petro..
Utawala wa Roma unakisia takriban watu millioni mbili wakiwemo viongozi 100 kutoka mataifa mbali mbali kuhudhuria mazishi ya baba mtakatifu ambae alifariki akiwa na umri wa miaka 84.
Katika muda wa wiki mbili zijazo makadinali wanatarajiwa kuanza harakati za maandalizi ya kumchagua kiongozi wa kanisa katoliki.