VATICAN-Baba Mtakatifu hatojiuzulu licha ya hali yake kuondelea kudhoofika.
31 Machi 2005Licha ya kuwa hali ya baba Mtakatifu Yohanne Paulo wa pili sio njema sana,viongozi katika makao makuu ya Baba Mtakatifu mjini Vatican,wameeleza kuwa kiongozi huyo wa Wakatoliki duniani hatojiuzulu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na Vittorio Messori katika gazeti la leo mjini Roma,vyovyote itakavyokuwa kwa hali ya afya yake,Baba Mtakatifu hatofikia uamuzi wa kujiuzulu.
Messori amesema Baba Mtakatifu,ataacha hatamu ya kuliongoza kanisa katoliki duniani ,pale tu atakapoitwa na Mungu.Messori ni mwandishi wa vitabu kadhaa katika kanisa Katoliki la Roma na amesema anayaeleza hayo kutokana na maagizo aliyopewa na viongozi wa juu wa Vatican.
Makao makuu ya Baba Mtakatifu yametangaza kuwa kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani mwenye umri wa miaka 84,hivi sasa analishwa kwa kutumia mirija iliyopitishwa puani na wamekiri kuwa anapona polepole mno.
Baba Mtakatifu ameeonekana kupungua uzito na amekuwa akipata shida ya kuzungumza mbele ya watu wanaofurika kumtakia afya njema,tangu alipotolewa hospitalini tarehe 13 mwezi huu,baada ya kufanyiwa upasuaji wa koo ya kumuondolea shida ya kupumua.