Vance asema Marekani inatafuta "amani ya kudumu" kwa Ukraine
15 Februari 2025Matamshi hayo yananuwia kupunguza mashaka miongoni mwa washirika wa Ukraine juu ya mpango wa Marekani wa kumaliza vita vinavyoendelea.
Vance ametoa matamshi hayo wakati wa mazungumzo yake ya kwanza na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Usalama wa mjini Munich.
Kiongozi huyo amesema Marekani imedhamiria kufanikisha amani ya kudumu itakayozuia mizozo mashariki mwa Ulaya miaka inayokuja.
Washirika wa Ukraine hasa barani Ulaya wameingiwa wasiwasi tangu Rais Donald Trump alipotangaza kwamba mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine yataanza hivi karibuni baada ya kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Rais Vladimir Putin wa Urusi pamoja na Zelensky.
Wengi wanahofia Marekani inaweza kufikia makubaliano na Urusi bila kuishirikisha kikamilifu Ukraine wala kuihakikishia usalama wa kudumu.
Katika mazungumzo ya mjini Munich, Zelensky amesema yuko tayari kwa juhudi za kumaliza vita kwa misingi ya kupatikana amani ya kudumu na usalama wa nchi yake.