Uzinduzi wa wiki ya ubunifu wa teknolojia ya kijani Tanzania
13 Februari 2025Wiki ya ubunifu wa Teknolojia ya Kijani inafanyika Tanzania ambapo kampuni za Kijerumani zinazofanya kazi nchini hapa na kampuni za Kitanzania zikitumia wasaa huo kubadilishana utaalamu katika upatikanaji wa masoko na ubunifu wa kiteknolojia ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa rasilimali ya maji na mifumo ya majitaka.
Hayo yanafanyika wakati takwimu zikionyesha kuwa, watu bilioni 2 duniani, hawana uhakika wa kupata maji safi na salama ya kunywa na kwa hapa nchini ikielezwa kuwa, karibu theluthi ya watu hawana uhakika wa maji safi ya kunywa, na nusu ya wakaazi ndio wanaweza kupata maji salama ya kunawa mikono.
"Tunaweza kumaliza madhara ya mabadiliko ya tabia nchi"
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa wiki ya teknolojia bunifu jijini hapa, Balozi wa Ujerumani Tanzania, Thomas Terstegen amesema Ujerumani ipo tayari kushirkiana na Tanzania katika kutumia teknolojia bunifu ili kuimarisha sekta ya maji.
''Teknolojia hizi za kijani, zinafanya kazi muhimu ya kuangazia changamoto katika sekta ya maji, kwa kutumia teknolojia hizi tunaweza kumaliza madhara ya mabadiliko ya tabia nchi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa maji.'', alisema Terstegen
Balozi Terstegen amesema kwa kupitia Jukwaa hilo ubadilishanaji wa utaalamu kati ya kampuni za Ujerumani na Tanzania utafanyika, na hivyo kuleta ushirikiano wenye manufaa, upatikanaji wa masoko mapya, na rasilimali za pamoja.
Changamoto ya upatikanaji wa maji safi
Kwa upande wake, Luisa Scheuber, Naibu Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Ubalozi wa Ujerumani, Dar es Salaa amesema kuwa nchi hizi mbili ni rafiki wa karibu.
''Ujerumani na Tanzania zina ushirikiano wa muda mrefu katika masuala kwa miaka zaidi ya 40 tulichoona ni kuwa uwekezaji mkubwa unahitajika katika kuimarisha sekta ya maji kuimrisha maji na majitaka Tanzania, lakini pia uwezeshaji wa rasilimali watu na taasisi katika sekta ya maji unahitajika'', alisema
Scheuber amesema kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na mifumo ya maji taka Tanzania na kueleza kuwa Idadi kubwa ya watu wanatembea umbali mrefu kupata maji na wakati mwingie katika hali isiyo ya usalama, na hali hii huathiri maisha hasa kwa wanawake na watoto
Wiki ya Ubunifu wa Teknolojia ya Kijani kati ya Ujerumani na Tanzania ni sehemu ya Mpango wa Ubunifu wa Teknolojia ya Kijani wa Ujerumani na Tanzania kwa ajili ya uwezeshaji wa kisasa wa sekta ya maji na majitaka. Mpango huu unatekelezwa na Ujumbe wa Sekta ya Viwanda na Biashara wa Ujerumani kwa Afrika Mashariki kupitia chombo chake cha huduma, AHK.