Uwiano baina ya marais wa Marekani na Iran
29 Juni 2005Bwana Juan Cole mwalimu wa historia katika chuo cha Michigan, nchini Marekani, wiki iliyopita alisema kwamba mfumo wa kampeni za marais hawa wawili zinaonyesha kwamba kuna uwiano baina yao. Haswa katika masuala ya wao kupendwa na watu, fikra zao juu ya serikali zao na matumaini yao katika uchaguzi kupitia watu wenye msimamo mkali wa kidini.
Wanafanana hata katika historia zao binafsi, hawajali kuhusu dunia, bali nchi zao tu na kwa maoni yao ni rahisi kutafautisha marafiki na maadui na pia mazuri na maovu.
Lakini pia kuna tofauti muhimu baina yao. Rais Bush alizaliwa kwenye familia ya kitajiri, wakati Rais Ahmedinejad alizaliwa kwenye mazingira tofauti na Baba yake alikuwa mhunzi.
Kwa sasa Rais Bush anauwezo mkubwa kuliko rais wa Iran, haswa katika masuala ya mahusiano na nchi za kigeni, yanayoongozwa nchini Iran na kiongozi mkuu wa kidini Ali Khameini. Alionyesha kufurahi kwa kuchaguliwa kwa Rais Ahmedinejad.
Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanasema, kauli za Rais Bush kushutumu uchaguzi wa Iran na kuunga mkono mgomo wa wanafunzi, zinawezekana kuwa sababu ya watu wengi kuwenda kupiga kura. Pia sio ajabu zilimsaidia Rais Ahmedinejad ashinde uchaguzi.
Waziri wa Masuala ya Ujasusi Ali Yunesi alimshukuru Rais Bush hadharani kwa kauli zake, ambazo zilikuwa zikionyeshwa mara kwa mara na televisheni ya serikali siku ya uchaguzi. Kauli za Rais Bush dhidi ya uchaguzi zilitumika na Rais Ahmedinejad kumpinga mpinzani wake wakati wa kampeni.
Mpinzani wake, rais wa zamani Ali Hashemi Rafsanjani, alisema serikali ya Iran inatakiwa kutafuta njia ya kuanza mazungumzo na serikali ya Marekani.
Wakati akiongea na wandishi wa habari rais huyo wa Iran alisema ukisikiliza kauli za Rais Bush basi utaelewa kwamba anatafuta ugomvi na Iran.
Bwana Cole alionyesha baadhi ya usawa katika masuala ya kisisa ya viongozi hawa wawili. Rais Ahmedinejad, sawa na Rais Bush, kamwe hawashambuli wapinzani wake mwenyewe, lakini hazui wafuasi wake kueneza uongo na kutumia mbinu nyingine za udanganyifu dhidi ya wapinzani wao wakati wa kampeni za uchaguzi.
Wote walikampeni kama wakombozi wa watu wa kawaida, ingawa walikuwa wanaungwa mkono na matajiri wakubwa. Kwa upande wa rais wa Iran, kwa mujibu wa Bwana Cole, aliungwa mkono na viongozi wa kidini walio mabilionea ambao hawajafanya lolote kwa ajili ya watu wa kawaida. Naye rais wa Marekani aliungwa mkono na watu wa biashara.
Marais wote wili walishambulia baadhi ya taasisi za serikali zao, ingawa nao walihusika katika taasisi hizo. Kwa mujibu wa Bwana Cole, Rais wa Iran anayemuunga mkono Khameini alilalamika kuhusu ufisadi na mambo mengine yaliopinga serikali na watu wa kawaida wakakubaliana naye na kumchagua.
Naye Rais wa Marekani mara nyingi anapenda kujionyesha kama sio mkazi wa mji wa Washington, makazi ya serikali yake na pia anaikosoa serikali hiyo mara kwa mara.
Rais Ahmedinejad alifaidika na kuungwa mkono na mashehe wa misikitini nchini kote pamoja na wanachama wa kikundi cha wanamgambo cha Basij. Kikundi cha Basij kina mashina ya kitaifa na waliongeza idadi ya wapiga kura, haswa katika maeneo ya vijijini na kwenye majimbo maskini. Pia Rais Bush anategemea sana wanachama wa makanisa yenye msimamo mkali wa kidini.
Profesa Gary Sick, mtaalam wa masuala ya Iran wa chuo cha Colombia, naye anakubali kuna umuhimu wa kulinganisha maraisi hawa wawili. Sio kwa sababu nchi zao zinafanana, lakini ili kuweza kufahamu kinachoendelea katika siasa na matokeo yake.