Ongezeko la ushuru lazua wasiwasi Uingereza
9 Septemba 2025Vyombo vya habari nchini Uingereza vinaripoti kuwa uamuzi wa waziri wa fedha Rachel Reeves wa kufikiria na kutangaza uwezekano wa kuweka ushuru mpya kwenye mauzo ya nyumba, kupanua maeneo ya ushuru wa mapato, mabadiliko kwenye msamaha wa pensheni, na na pia uwezekano wa kuanzisha ushuru zaidi kwa benki na michezo ya bahari nasibu umeleta mkanganyiko kwa wananchi. Matarajio haya yanatazamiwa kutangazwa wakati wa kusoma bajeti hiyo nchini Uingereza mnamo Novemba 26.
Uingereza iliongoza katika kundi la nchi saba matajiri G7 katika ukuaji wa kiuchumi kwenye nusu ya kwanza ya mwaka 2025, na kiwango cha ukuaji huo kilitokana na matumizi makubwa ya umma na kuongeza uzalishaji wa viwandani kwa lengo la kuepuka ushuru wa Marekani.
Hata hivyo licha ya ukuaji huo bado kiasi cha fedha kwa matumizi ya umma kimesalia kuwa katika hali isiyotabirika, suala ambalo wadadisi wa kiuchumi wanakadiriwa kuwa waziri wa fedha Rachel Revees anatakiwa kukusanya pauni billion kati ya 20 hadi 40 ili kufikia kiwango cha pesa inayotakiwa.
Shirikisho la mashirika ya viwanda nchini Uingereza limeiasa serikali ya nchi hiyo isirudie tena kitendo cha mwaka jana cha kupandisha ushuru wa wafanyakazi likionya kwamba hali ya kukosa uhakika kwa muda kwa sasa tayari imeshasabisha kupotea kwa imani katika sekta ya uwekezaji na huduma kwa jamii.
Mazungumzo kuhusu uwezekano wa kupandisha ushuru kumesababisha hofu na mashaka
Watalaam kutoka taasisi ya uchunguzi kuhusu ushuru Institution of Chartered Surveyors wanasema kuendelea kwa kauli na mazungumzo kuhusu uwezekano wa kupandisha ushuru kumesababisha hofu na mashaka makubwa kwa kiwango cha juu na kwa mara ya kwanza tangu kutokea kwa janga la COVID-19. Hali hii huenda ikasababisha kushuka kwa bei za nyumba suala ambalo wengi wanaliona kama onyo kuhusu hali tete siku za usoni.
Kwa upande mwinginekampuni ya Brightmine ambayo hufanya tathmini kwa malipo ya wafanyakazi imesema kwamba sekta binafsi huenda isipandishe malipo kwa makazi ambayo kwa sasa yapo chini ya kiwango cha mfumuko wa bei hadi pale hali ya msimamo wa bajeti utakapokuwa wazi nchini Uingereza.
Kwa sasa lakini inaelekea kwamba waziri wa fedha Rachel Reeves hatarudia kuweka ongezeko kubwa la ushuru kama ilivyofanyika katika bajeti ya mwaka jana ambalo lilikuwa kubwa zaidi katika miongo mitatu iliyopita.
Hata hivyo, hadi sasa serikali ya Uingereza inakabiliwa na vurugu. Waziri Mkuu Keir Starmer aliondoa mpango wa kuweka akiba kubwa za huduma za jamii mwezi Juni, na shirika la ufuatiliaji wa sera za fedha linatarajiwa kupunguza makisio ya ukuaji, jambo litakaloathiri mapato ya baadaye ya ushuru.
Wadadisi wa kiuchumi wanatabiri kuwa waziri Reeves hana chaguo jingine isipokuwa kuongeza ushuru ili kusawazisha matumizi ya kila siku na mapato kabla ya mwisho wa muongo huu, au kinyume chake akose imani ya masoko ya dhamana.
Wataalamu wanadai pia kuwa ni muhimu kurekebisha mfumo wa kifedha ili kuleta uhakika na kuboresha mazingira ya uwekezaji hasa endapo hali ya usumbufu wa kulegalega mfumo wa fedha utaendelea kuyumba.
Masoko ya hisa kwa upande mwingine yameendelea kuwa katika hali ya tahadhari tangu mwaka 2022 wakati wa utawala wa waziri mkuu Liz Truss wakati bajeti ndogo wakati huo ilipokumbwa na msukosuko. Wiki hii kiwango cha kukopa katika hisa za serikali kwa dhamana ya miaka 30 kimepanda zaidi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998. Hali hii imewafanya wadadisi wa kiuchumi kushauri kuwa kunatakiwa marekebisho makubwa kuhusu kanuni na sheria kuhusu bajeti.
Stephen Millard kutoka taasisi ya kiuchumi na utafiti ameonya” kama unataka makampuni kuwekeza, zingatia kuwa wao pia wanahitaji uhakika wa kile kitakachotokea katika miaka michache ijayo” mwisho wa kumnukuu.
Kwa hali hii wadadisi wa kiuchumi wanasema hawana uhakika ikiwa waziri wa fedha Rachel Revees ana uwezo zaidi wa kupanua wigo wa ushuru zaidi kwa sababu kwa kufanya hivyo atajikuta anazidi kuharibu zaidi, suala ambalo wanasema limemuacha njia-panda