Uturuki yawakamata wapinzani wa Erdogan Izmir
1 Julai 2025Polisi wa Uturuki wamewakamata watu zaidi ya 120 katika mji ulio ngome ya upinzani wa Izmir, saa chache kabla mkutano muhimu mjini Istanbul, katika hatua ya hivi karibuni inayowalenga wapinzani wa rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdogan.
Naibu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha CHP, Murat Bakan, amesema meya wa zamani na maafisa kadhaa waandamizi ni miongoni mwa waliotiwa mbaroni huko Izmir, mji wa tatu kwa ukubwa, ambao upinzani umekuwa ukiutawala kwa miaka.
Ukamataji huo wa asubuhi na mapema umefanyika kufuatia operesheni inayofanana na hiyo katika mji unaoendeshwa na upinzani wa Istanbul mnamo mwezi Machi iliyomuondoa na kumtia gerezani meya Ekrem Imamoglu, mpinzani mkuu wa Erdogan katika uchaguzi wa uraisi uliopangwa kufanyika mwaka 2028.