Uturuki yawafunga waandishi, waandamanaji wazidi kukaidi
26 Machi 2025Waandamanaji nchini Uturuki waliingia mitaani kwa siku ya sita mfululizo Jumanne, huku waandishi saba wa habari wakikamatwa katika operesheni kubwa ya kudhibiti upinzani.
Machafuko hayo nchini Uturuki yalianza baada ya meya wa Istanbul Ekrem Imamoglu, ambaye ni mpinzani mkuu wa kisiasa wa Rais Recep Tayyip Erdogan, kukamatwa wiki iliyopita akituhumiwa kwa ufisadi.
Kukamatwa kwa Imamoglu kulichochea maandamano ambayo yalifuatiwa na ukandamizaji uliosababisha zaidi ya watu 1,400 kukamatwa.
Miongoni mwa waandishi waliokamatwa ni mpiga picha wa AFP Yasin Akgul. Waandishi hao walikabiliwa na mashtaka ya "kushiriki katika mikutano na maandamano haramu," ingawa AFP imesema Akgul "hakuwa sehemu ya maandamano," bali alikuwa akiripoti kama mwandishi wa habari.
Soma pia: Takriban waandamanaji 1,100 wakamatwa na polisi Uturuki
"Kukamatwa kwake hakukubaliki kabisa. Ndio maana ninakuomba uingilie kati haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha mwandishi wetu anaachiliwa haraka," Mkurugenzi Mtendaji wa AFP Fabrice Fries alisema katika barua kwa ofisi ya rais wa Uturuki, akilaani vikali kitendo hicho.
Maelfu waliandamana kupitia wilaya ya Sisli mjini Istanbul Jumanne, wakielekea ofisi za manispaa wakitaka serikali ijiuzulu.
Waandamanaji walipeperusha bendera na mabango yenye kauli mbiu kama "Tayyip jiuzulu!" huku wakazi wa majengo wakipiga sufuria na vyombo vingine kuunga mkono maandamano hayo.
Erdogan asema maandamano yatakwama
Kuhusu kukamatwa kwa Imamoglu, serikali ya Uturuki imekanusha madai ya ushawishi wa kisiasa na kusisitiza kwamba mahakama ya nchi hiyo ni huru.
Erdogan amekishutumu chama kikuu cha upinzani cha Republican People's Party (CHP) kwa kuchochea wananchi, akisema wataona aibu kwa "maovu" waliyoyafanyia nchi mara tu "maonyesho" yao yatakapoyeyuka.
Akizungumza na kundi la vijana katika futari ya mwezi wa Ramadhani siku ya Jumanne, rais wa Uturuki aliwataka watu wawe na subira na busara katika siku hizi ambazo aliziita kuwa "nyeti sana."
"Wale wanaovuruga mitaa yetu na wanaotaka kuigeuza nchi hii kuwa eneo la machafuko hawana pa kwenda. Njia waliyoichukua ni ya kukwama," Erdogan alisema.
Upinzani waitisha maandamano makubwa
Kiongozi wa CHP, Ozgur Ozel alimtembelea Imamoglu katika gereza la Silivri, magharibi mwa Istanbul. Ozel aliwaambia waandishi kwamba anajisikia "aibu kwa niaba ya wale wanaotawala Uturuki kutokana na hali iliyopo na mazingira ambayo Uturuki inapitia."
Ozel alisema Imamoglu pamoja na mameya wengine wawili wa wilaya kutoka CHP waliokamatwa ni "simba watatu, wenye msimamo thabiti, vichwa juu, wakijivunia wao wenyewe, familia zao, na wenzao, bila woga."
Alisema CHP itamteua kaimu meya kushika nafasi ya Imamoglu ili kuepuka uteuzi kutoka serikali kuu.
Ozel amewataka wananchi wote wa Uturuki kushiriki maandamano makubwa siku ya Jumamosi mjini Istanbul.
"Je, mko tayari kwa maandamano makubwa kwenye uwanja mkubwa mjini Istanbul Jumamosi ili kumuunga mkono Imamoglu, kupinga kukamatwa kwake, kudai kesi za wazi na za haki, kusema tumechoshwa na tunataka uchaguzi wa mapema?" Ozel aliuliza waandamanaji Jumanne.
Maandamano ya Jumamosi yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vikubwa vya Maltepe, upande wa Asia wa Istanbul.